TGNP KUFANYA MAPITIO YA SERA NA ILANI ZA VYAMA VYA SIASA TANZANIA



Na Deogratius Temba - Dar es salaam
TGNP Mtandao imepanga kufanya mapitio ya sera na ilani za vyama vya siasa kwa mrengo wa kijinsia na kushauri kufanya marekebisho mapema kabla ya uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Akizungumza leo wakati wa ziara ya kukabidhi ilani ya madai ya wanawake katika uchaguzi wa serikali za Mitaa wa mwaka 2019 na uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 kwa chama cha ACT Wazalendo, Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP Mtandao Lilian Liundi, amesema baada ya kutembelea vyama kadhaa vya siasa nchini na kusikiliza jinsi wanavyotekeleza masuala ya kijinsia, ameona kuwa kuna haja ya TGNP na Mashirika mengine yanayotetea haki za wanawake na Usawa wa Jinsia, kufanya uchambuzi au mapitio ya sera na ilani za vyama kwa mrengo wa kijinsia na kuangalia mapengo ili kushauri marekebisho.

“Tunapoelekea uchaguzi wa serikali za Mitaa, na uchaguzi mkuu mwaka ujao 2020, tunahitaji vyama hivi kuzingatia kwa kiasi kikbwa usawa wa kijinsia kwneye uteuzi wa wagombea. Kama chama hakina sera za ndani ambazo zina mrengo wa kijinsia, ni lazima mapendo yataendelea kuwepo. Tunashukuru kwamba vyama vya siasa vimejitahidi, lakini bado hatujafikia malengo”, amesema. 

Kwa upande wake Kaimu Mwenyekiti Chama Cha ACT Wazalendo Doroth Semu amesema pamoja na kwamba chama kinajitahidi kutoa fursa sawa kwa wanawake bado watajitahidi kuendelea kuteua wanawake kushiriki kwenye chaguzi.

“Mwaka huu tumejipanga kwenye uchaguzi wa serikali za Mitaa, tutahakikisha kila mahali ambapo wanawake wamejitokeza wanapata nasi, lakini kwa sababu mmetuletea hii Ilani yenu, tutahakikisha tunaitumia ili wagombea watakao shinda wakatekeleze ilani husika”, amesema Semu.

Ilani ya Madai ya wanawake kwa uchaguzi wa serikali za Mitaa 2019 na Uchaguzi Mkuu 2020 iliyoandaliwa na TGNP Mtandao kwa kushirikiana na Mtandao wa wanawake na Katiba, imewashirikia na kukusanya maoni ya wanawake kutoka katika makundi yote nchini hasa vijijini.

Asasi za kiraia zinazotetea haki na usawa wa Kijinsia zaidi ya 60 zimeshiriki.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527