RAIS MAGUFULI AKAGUA MAENDELEO YA UJENZI WA CHELEZO NA UKARABATI WA MELI 5 ZA ZIWA VICTORIA KATIKA BANDARI YA MWANZA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ametoa siku 5 kuanzia leo July 16, 2019 kwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na Wizara ya Fedha na Mipango kuhakikisha vifaa vya ujenzi wa chelezo ya kujengea meli na vifaa vya ukarabati wa meli vilivyokwama katika Bandari ya Dar es Salaam kutokana na mchakato wa kikodi vinafikishwa katika Bandari ya Mwanza.


Rais Magufuli ametoa agizo hilo alipotembelea Bandari ya Mwanza kwa lengo la kukagua maendeleo ya ujenzi wa chelezo, ukarabati wa meli 5 na ujenzi wa meli mpya katika Ziwa Victoria yanayofanywa na kampuni 2 za ukarasi kutoka Jamhuri ya Korea kwa gharama ya shilingi Bilioni 152 kwa ajili hiyo.

Akiwa bandarini hapo, Rais Magufuli ameeleza kutofurahishwa na ucheleweshaji wa takribani mwezi mmoja wa makontena 58 yenye vifaa vya ujenzi vilivyoagizwa na kampuni za ukandarasi za Korea Total Marine Innovation (KTMI) na STX JV SAEKYUNG Construction Ltd za Korea kwa sababu ya kusubiri msamaha wa kodi na amemtaka mkandarasi huyo aache visingizio.

Meneja wa mradi wa ujenzi wa chelezo na ukarabati wa meli Mhandisi Abel Gwanafyo amesema ujenzi wa chelezo pamoja na ukarabati wa meli ya MV Victoria na Mv Butiama umepangwa kukamilika ifikapo Machi 2020.

Kuhusu ujenzi wa meli mpya Meneja Mradi wa ujenzi wa Meli hiyo Mhandisi Vitus Mapunda amesema maandalizi ya vifaa vya meli hiyo itakayokuwa na uwezo wa kubeba tani 400 za mzigo, abiria 1,200 na magari makubwa na madogo 23 yanayohusisha usanifu, ukataji wa vyuma, injini 2 na majenereta 3 yamefikia asilimia 35 na kwamba makontena 300 yenye vifaa hivyo yatawasili nchini Septemba 2019 kutoka nchini Korea.

Baada ya kukagua hali ya meli ya Mv Victoria na Mv Butiama ambazo ukarabati wake umeanza, Rais Magufuli namewasalimu wafanyakazi walioajiriwa katika mradi huo na kuwaagiza wakandarasi kuhakikisha wanalinda maslahi yao na sheria za usalama kazini kuzingatiwa.

Pia Rais Magufuli ameagiza mitambo miwili ya kunyanyulia mizigo (Cranes) iliyokuwa imeuzwa na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kurejeshwa mara moja.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527