WAZEE WA CHADEMA WATUMA MAOMBI YA KUONANA NA RAIS MAGUFULI


Baraza la Wazee Chadema limesema Rais Dk. John Magufuli anapaswa kukutana na viongozi wa vyama vya upinzani kama alivyofanya kwa viongozi wa dini na wafanyabiashara.


Kauli hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Chadema, Hashim  Juma Issa alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.

Issa ambaye alizungumzia mambo mbalimbali ikiwamo Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, matumizi fedha za umma na hali ya kisiasa nchini, alisema Rais aondoe wasiwasi na akutane na viongozi wa vyama vya upinzani wa juu kila chama ili aweze kubadilishana nao mawazo.

“Ameshakutana na viongozi wa dini alifanya jambo la maana sana…tunajua umekutana na wafanyabiashara hongera sana, hivyo ndivyo unavyotakiwa uwe kiongozi wa nchi.

“Lakini kwa bahati mbaya sana, sijui kwa nini hujakutana na viongozi wa vyama vya upinzani tangu umeingia madarakani, hapo unakuwa hutendi haki,”alisema Issa.

“Waambie kila chama angalau kije na viongozi 10 wa juu, tuje hapo, tukukosoe mbele yako, ndani  ya ikulu yako, tukueleze kasoro zako kama utaweza ujirekebishe,” alisema.

Mwenyekiti huyo wa Baraza la Wazee alikumbusha majibu yaliyowahi kutolewa na Rais Magufuli wakati akipokea ndege baada ya kushauriwa na kiongozi wa mmoja wa dini kuhusu kuonana na wapinzani, ambapo alisema hawezi kuonana nao kwa sababu wana njama za kumuhujumu.

 “Sisi kama Baraza la Wazee tukwambie, kitu kama hicho hakipo Chadema, na nina amini hata kwa vyama vingine hakipo ingawa mimi sio msemaji wa vyama vingine lakini naamini kitu kama hicho hakuna.

“Sisi Chadema hatuna nia ya kukudhuru wewe, hatuna nia ya kumdhuru mtu yoyote yule, wala hatuna kisasi chochote”

“Hata mfano ikitokea Mungu akijalia  tumeshinda uchaguzi 2020, sisi tunafuta mambo yote yaliyotokea nyuma, hatutomuhukumu mtu yoyote, hatutofukua makaburi yoyote wala hatuna kisasi na mtu yoyote,” alisema.

Kuhusu Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Mwenyekiti huyo wa Baraza la Wazee alisema wamejiandaa kushiriki kwa asilimia 100.

“Tunamwambia Mwenyekiti wa CCM, Katibu Mkuu kuwa safari hii Baraza la Wazee tunakula kiapo hatutokubali kwa namna yoyote ile kuibiwa kura hata moja.

“Tunasikia Rais ameteua wakurugenzi na tunasikia tetesi kwamba baadhi ya vituo vitawekwa kwenye kambi za jeshi

“Sasa sisi kama Baraza la Wazee kwa sababu tunajiamini na tunadhamira safari hii kuingia kwenye uchaguzi hata waweke ma-DED  wa aina gani, vituo vyote vya Tanzania  viwe ndani ya kambi za jeshi, viwe ndani ya vituo vya  polisi,  viwe ndani jela za magereza na hata vingine vikiwekwa mochwari sisi tunaingia humo humo, tutapiga kura  tutashinda humo humo na hatutaibiwa kura hata moja”alisema.Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post