SERIKALI YAAHIDI KUFANYA KAZI NA VIJANA KATIKA UTEKELEZAJI WA SERA YA KILIMO

Najma Khamis Salum, Afisa mawasilianao - Sahara Consulting Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imesema ipo tayari kufanya kazi na Vijana wabunifu katika utekelezaji wa Sera yake mpya ya Kilimo nchini ambapo suala la matumizi ya Teknolojia katika kilimo limepewa kipaumbele.Hayo yamesemwa na Katibu MKuu wa Wizara ya Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe juzi tarehe 2 Julai 2019 wakati wa kikao maalumu kilicho itishwa na Wizara hiyo kupata ufahamu zaidi kuhusu mradi wa E-Kilimo Accelerator uliojikita katika kutafuta suluhu za teknolojia za kidijitali zinazosaidia kupambana na changamoto mbalimbali kwenye sekta ya kilimo.

Mradi huo wa E-Kilimo Accelerator umefadhiliwa na ubalozi wa Denmark nchini na kuendeshwa na Shirika la Sahara Consulting la jijini Dar es salaam.

Akizingumza katika kikao hicho kilichowahusisha wataalamu wa ngazi za juu wa Wizara ya Kilimo kutoka vitengo vyake vyote, Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara hiyo Bw. Assery Obey amesema, Serikali ingependa kuona bunifu hizo zilizopatikana kupitia mradi huo zinatumika ipasavyo kwa kushirikiana na Wizara katika kutatua changamoto mbalimbali na ikiwezakana kufanya kazi na vitengo vyake katika kuziendeleza na kuzitumia katika maeneo yake ya utekelezaji.

“Nimefurahishwa na jinsi kampuni hizi zilivyokua zikiwakilisha bunifu zao hapa na vile walivyoweza kuchambua maeneo ya vipaumbele ya serikali na kupendekeza jinsi gani wanaweza kufanya kazi na Serikali”. Alisema  Assery.

Serikali pia imetoa wito wa ushirikwashaji wa serikali wakati wa uandaaji miradi hiyo na usimamiaji ili kuhakikisha inaleta matokeo makubwa zaidi na inajibu changamoto husika.

Nae Bwana Adam Mbyallu ambae ni Mkuregenzi wa Shirika la Sahara Consulting ambayo ni miongoni mwa taasisi tanzu ya Sahara Ventures ameishukuru Wizara ya Kilimo kwa utayari wake wa kufanya kazi na vijana na kuona bunifu zao zinaendelezwa.

“Sio lazima kila kijana ajihusishe na Kilimo kwa maana ya kulima moja kwa moja, Vijana kwa taaluma zao wanaweza wakabuni namna bora ya kusaidia Mnyororo wa Kilimo kupitia bunifu na teknolojia mbalimbali”. Alisema Bw, Mbyallu.

Mkutano huo, ulihudhuriwa pia na Mwakilishi kutoka Ubalozi wa Denmark nchini Tanzania Bw. Boniface Ihunyo.

Kwa upande wake Bw. Ihunyo amesema Ubalozi wa Denmark nchini uliamua kusaidia mradi huu katika juhudi zake za kuangalia ni kwa namna gani teknolojia inaweza kusaidia katika nyanja mbalimbali nchini ambapo kilimo ni moja ya nyanja kuu na hivyo basi kuona umuhimu wake.

Mradi huu ni wa kwanza na wa kipekee  unahusisha kusaidia ongezeko la kasi la biashara za kilimo. E-Kilimo ililenga kuongeza kasi katika ukuaji wa sekta ya bidhaa za chakula na mazao Tanzania kupitia matumizi ya teknolojia na uvumbuzi katika utatuzi wa changamoto zinazoikumba sekta hiyo na hivyo kuleta matokeo katika uzalishaji, ajira na fursa za maendeleo.

Jumla ya bunifu Tisa zimeweza kupatikana katika mradi huo na tano kati ya hizo ziliweza kuwasilisha bunifu hizo Wizarani.

Miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa katika mkutano huo ni pamoja na yafuatayo;
●     Ni kwa namna gani kwa pamoja tunaweza kushirikiana ili kuweza kumsadia mkulima mdogo.
●     Ni kwa namna gani tunaweza kushirikiana kuandika na kuandaa miradi ya kilimo.
●     Na pia jinsi ya kuwasaidia vijana wanaokuja na mawazo mbalimbali ya kibunifu.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post