KUBORESHWA KWA MIUNDOMBINU SKIMU ZA UMWAGILIAJI KWAPAISHA BAJETI YA HALMASHAURI MVOMERO MKOANI MOROGORO

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mvomero,Mhe.Florent Kyombo akifafanua jambo ofisini kwake mbele ya Kaimu Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji,Bwa.Marco Ndonde, Mkurugenzi wa Uendelezaji Miundombinu -Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Mhandisi Senzia Maeda wakiwa na Wataalamu pamoja na Wafanyakazi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (hawapo pichani),kuhusu Skimu ya Umwagiliaji wilayani humo mkoani Morogoro
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mvomero,Mhe.Florent Kyombo akisoma moja ya kitabu (nyenzo) kinachohusu Skimu ya mwagiliaji,alichokabidhiwa na Kaimu Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji,Bwa.Marco Ndonde (pichani kulia) kwa ajili ya kuendelea kuimarisha Skimu ya Umwagiliaji Wilayani humo,mkoani Morogoro.

Tume ya Taifa ya Umwagiliaji,Wataalamu wapo katika wilaya hiyo ya Mvomero kupata taarifa kuhusu Maendeleo na mafanikio waliyoyapata baada ya ukarabati mkubwa wa miundombinu kufanyika katika shamba la Ushirika la Wakulima Wadogowadogo Kilimo cha Umwagiliaji Mpunga Dakawa (UWAWADA),Wilayani humo,ambapo ukarabati wa miundominu hiyo umefadhiliwa na Serikali ya watu wa Marekani kupitia Shirika la Misaada la USAID-Tanzania,aidha gharama za ufadhili huo wa Ukarabati wa Miundombinu hiyo ya shamba imegharimu zaidi ya Shilingi bilioni 24.
Pichani kulia Kaimu Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji,Bw.Marco Ndonde na kushoto ni Mkurugenzi wa Uendelezaji Miundombinu -Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Mhandisi Senzia Maeda wakiwa na Wataalamu pamoja na Wafanyakazi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji wakimsikiliza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mvomero,Mhe.Florent Kyombo kwa ajili ya kupata taarifa kuhusu Maendeleo na mafanikio waliyoyapata kufuatia ukarabati mkubwa wa miundombinu uliofanywa katika shamba la Ushirika la Wakulima Wadogowadogo Kilimo cha Umwagiliaji Mpunga Dakawa (UWAWADA),Wilayani humo,ambapo ukarabati wa miundominu hiyo umefadhiliwa na Serikali ya watu wa Marekani kupitia Shirika la Misaada la USAID-Tanzania,aidha gharama za ufadhili huo wa Ukarabati wa Miundombinu hiyo ya shamba imegharimu zaidi ya Shilingi bilioni 24. 
Mkurugenzi wa Uendelezaji Miundombinu -Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Mhandisi Senzia Maeda akiomba taarifa kutoka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mvomero,Mhe.Florent Kyombo kuhusu Skimu ya Umwagiliaji katika Wilaya ya Mvomero inavyofanya kazi na mafanikio yake mpaka sasa.
Kaimu Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji,Bwa.Marco Ndonde (kushoto) pamoja na Wataalamu kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji wakifuatilia taarifa iliyokuwa ikitolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mvomero,Mhe.Florent Kyombo kuhusu maendeleo na mafanikio ya Skimu ya Umwagiliaji wilayani humo.
***

Na Ripota, Michuzi TV-Morogoro

HALMASHAURI ya Wilaya Mvomero mkoani Morogoro imesema asilimia 30 kati ya asilimia 33 ya bajeti ya halmashauri hiyo inategemea mazao ya kilimo na hasa cha umwagiliaji.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Florent Kyombo mbele ya Mkurugenzi wa Uendelezaji Miundombinu -Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Mhandisi Senzia Maeda pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Marco Ndonde.

Wakurugenzi hao wapo katika wilaya hiyo ya Mvomero kwa lengo la kuangalia shughuli za kilimo cha umwagiliaji kinachotokana na skimu zilizopo wilayani humo ikiwa ni jitihada za Serikali kuimarisha kilimo cha umwagiliaji.

Akifafanua zaidi Kyombo amesema mchango wa kipato kinachotokana na kilimo cha umwagiliaji kwa halmashauri ni mkubwa na asilimia 33 ya bajeti ya halmashauri inategemea mazao ya kilimo na kati hizo 30 ni mazao ya umwagiliaji.

"Hivyo tukiona skimu zinaendelezwa katika Wilaya yetu na zinafanya kazi kwa ufanisi tunaamini wananchi wetu watavuna sana na maana yake hata kwa halmashauri tunatajia mapato ya fedha za bajeti kuongezeka.

"Hivyo kupitia fedha hizo halmashauri itajenga madarasa, zahanati, itaboresha miundombinu pamoja na kuendeleza miradi mingine ya maendeleo kwa ajili ya wananchi,"amesema Kyombo.

Pia amesema kuimarika kwa miundombinu kumekuwa kukiongeza mzunguko wa fedha, kwani sehemu kubwa ya kipato cha wananchi kinategemea kilimo na mifumo. "Hivyo wananchi wakivuna utaona mzunguko wa fedha unaongezeka na shughuli za uchumi zinachangamka ikiwemo watu kwenda minadani."

Akizungumzia skimu katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Kyombo amesema kuna skimu 11 lakini zinazofanya kazi ni chache kwani nyingine bado hazijaendelezwa. 

"Ukiangalia hata maeneo yaliyowekwa miundombinu ni madogo ukilinganisha na ukubwa wa eneo la Skimu. Hata hivyo kupitia skimu hizo chache ukweli ni kwamba faida zake ni nyingi sana kwani kwa sasa uzalishaji wa zao la mpunga umeongezeka na hiyo maana yake pato la mwananchi nalo limeongezeka,"amesema Kyombo.

Amesisitiza kutokana na kuboreshwa kwa skimu hizo wakulima wa zao la mpunga wanavuna kati ya gunia 40 hadi gunia 50 kwa ekari moja wakati huko nyuma kabla ya skimu walikuwa wnavuna kati ya gunia 10 hadi 15 tu.

"Kuptia skimu ambazo tunazo , uzalishaji wa zao la mpunga umeongezeka.Pia imetoa fursa ya ajira kwa vijana, wanawake na wanaume na kubwa zaidi kila mmoja anaweza kujikwamua kiuchumi."Hivyo Halmashauri tumeendelea kuwa na mikakati ya kuomba fedha ili skiku ambazo bado hazijaendelezwa nazo ziendelezwe.Kwa Dakawa tunayo skimu kubwa sana ambayo uwepo wapo umefanya kuwe kunazalishwaa mpunga kwa wingi sana,"amesema Kyombo.

Pia amesema kwa halmashauri yao nao wamejipanga ili kuwa na Skimu ambayo wanaamini itasaidia kuongeza mapato na kuwa chachu kwa wakulima wa mpunga huku akitoa rai kuwa wananchi wanalo jukumu la kuhakikisha skimu ambazo miundombinu yake imeendelezwa inalindwa.Wakati huo huo ameipongeza Serikali kwa jitihada zake za kuendeleza skimu zilizopo Mvomero kwani imekuwa ikitumia fedha nyingi kuziendeleza ikiwemo skimu ya Dakawa.

Pia amesema kuna skimu nyingi ambazo nazo miundombinu yake ipo hatua mbalimbali ya kuendelezwa na ni matumaini yao zitakapokamilika zitasaidia kuongeza upatikanaji wa mazao ya kilimo."Wananchi wamehamasika sana kutokokana na uwepo wa skimu hizi.Tunafahamu skimu kongwe zote nazo zipo kwenye mchakato wa kuendelezwa ikiwemo skimu ya Mkenge ambayo imeshawekewa banio na itaanza kutumika siku za karibuni,"amesema Kyombo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527