KAMISHINA WA POLISI WAKULYAMBA AKAGUA UJENZI WA NYUMBA ZA ASKARI POLISI BUKOBA

Na Lydia Lugakila- Malunde1 blog Bukoba
Kamishina wa Polisi anayeshughulikia Masuala ya Utawala na Menejimenti ya Rasilimali Watu,Benedicto Michael Wakulyamba  ametembelea na kukagua nyumba za makazi ya askari polisi zinazojengwa katika  eneo la Rwamishenye Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera ambazo ujenzi wake unatarajiwa kukamilika mwezi huu.

Wakulyamba amefanya ziara hiyo leo Julai 16,2019 na kujionea jinsi ujenzi wa nyumba tatu ambapo kila jengo linachukua familia mbili na sasa ujenzi umefikia asilimia 95.

Wakulyamba aliyemwakilisha Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro  ametumia fursa hiyo kuwataka askari polisi kufanya kazi kwa weledi mkubwa.


Amesema kuwa askari polisi nchini wamekuwa wakikumbana na changamoto mbali mbali ikiwemo kutokuwa na makazi bora hivyo baada ya kuboreshewa makazi watafanya kazi kwa weledi mkubwa zaidi.

"Namshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu Mpendwa,Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutoa pesa kwa ajili ya kuboresha makazi ya askari polisi nchini,lakini pia tunawapongeza na kuwashukuru sana kamati ya ujenzi na wadau wote waliosaidia katika ujenzi wa makazi haya",ameongeza.

Naye Msimamizi wa ujenzi wa majengo hayo,Avit Teodory  amesema changamoto kubwa iliyofanya ujenzi huo kutomalizika kwa wakati kuwa ni mvua zilizonyesha kwa wingi mkoani Kagera.
Kushoto ni Kamanda wa jeshi la polisi mkoani Kagera Revocatus Malimi akimwelezea Kamishina wa Polisi Polisi anayeshughulikia Masuala ya Utawala na Menejimenti ya Rasilimali Watu,Benedicto Michael Wakulyamba  (katikati) kuhusu ujenzi wa nyumba za makazi ya askari polisi zinazojengwa katika  eneo la Rwamishenye Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera.
Kamishina wa Polisi Polisi anayeshughulikia Masuala ya Utawala na Menejimenti ya Rasilimali Watu,Benedicto Michael Wakulyamba  akiangalia nyumba za makazi ya askari polisi zinazojengwa katika  eneo la Rwamishenye Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527