WATUMISHI MAMBO YA NDANI ‘WAIKOSHA’ HOSPITALI YA MIREMBE, WAPEWA ELIMU

Na Mwandishi Wetu, MOHA

UONGOZI wa Hospitali ya Rufaa ya Wagonjwa wa Akili ya Mirembe, mkoani Dodoma, umefurahishwa na kitendo cha watumishi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwenda kufanya usafi wa mazingira hospitalini hapo.

Pongezi hizo zimetolewa na Kaimu Mganda Mkuu wa hospitali hiyo, Dkt. Escor Tweve. Watumishi hao wakiwa na baadhi ya viongozi wa Wizara, idara zilizopo chini ya Wizara hiyo, waliadhimisha Wiki ya Utumishi wa Umma kwa kufanya usafi wa mazingira hospitalini hapo.

“Nawashukuru kwa uamuzi wa kuja kufanya usafi wa mazingira hospitalini hapa kwa kufyeka, kulima, kuchoma taka, kudeki na kufanya kazi nyingine za kijamii. “Mmeonyesha upendo mkubwa mlionao dhidi yetu, mmejitoa kwa moyo wa dhati, miaka mingi imepita hatujawahi kupata ugeni uliofanya jambo muhimu kama hili,” alisema Dkt. Tweve.

Mbali ya kufanya usafi wa mazingira, watumishi hao walipata fursa ya kupewa elimu juu ya huduma zinazotolewa kwa wagonjwa hospitalini hapo.  Dkt. Tweve alisema changamoto kubwa waliyonayo wagonjwa wa akili huwa hawapendwi katika jamii ila ni watu wanaopaswa kupewa upendo mkubwa na jamii.

“Wagonjwa wa akili hawana tofauti na watu wengine ambao hawana matatizo kama yao kwenye jamii, wanapoletwa hapa hospitali huwa tunawapatia matibabu, kupona, kutoa michango mizuri kwenye jamii na nchi kwa ujumla,” alisema. 

Aliishukuru Wizara hiyo kwa ushirikiano mkubwa wanaowapa kwani kuna wagonjwa wengine wa akili hukamatwa, kuhitajika kufanyiwa matibabu hospitalini hapo.

Pia wapo baadhi ya watumishi wa idara za serikali wakiwemo askari ambao hospitali hiyo huwapatia matibabu ya akili, kupona, kuendelea na majukumu yao ya kazi. 

“Naishukuru Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuadhimisha siku hii kwa kuja Mirembe na kufanya usafi wa mazingira, nawaomba muwe na utaratibu wa kuja mara kwa mara,” alisisitiza.

Aliwapongeza watumishi wa Wizara hiyo na viongozi wao akiwemo Waziri Kangi Lugola, Naibu Waziri, Mhandisi Hamad  Masauni, Katibu Mkuu, Meja Jenerali Jacob Kingu, Naibu KaribuMkuu, Ramadhani kailima kwa utendaji mzuri wa kazi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha TEHAWA katika Wizara hiyo, Jane Massawe ambaye alimwakilisha Katibu Mkuu, aliushukuru uongozi wa hospitali hiyo kwa ushirikiano walioutoa kwa watumishi  hao. 

“Tumefurahishwa na mapokezi mliyotupa, tupatapo nafasi kwa siku nyingine tutakuja kuwatembelea na kufanya shughuli za kijamii,” alisema Massawe.

Wiki ya Utumishi wa umma ilianza huadhimishwa kuanzia Juni 17 hadi 22, mwaka huu. Maadhimisho hayo ni kwa mujibu wa Kalenda ya Umoja wa Afrika (AU).  Nchi mbalimbali huadhimisha siku hiyo kwa kushiriki shughuli mbalimbali zinazohusu utumishi wa umma.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post