WATAFITI WATAKIWA KUTUMIA MBINU ZA KISAYANSI ILI KULETA TIJA KATIKA JAMII

Na. Peter Haule na Farida Ramadhani WFM, Dodoma

Watafiti nchini wametakiwa kuweka mkazo katika mbinu za utafiti zinazokidhi viwango vya kimataifa ili kuwa na majibu ya tafiti zenye tija zilizo na lengo la kutatua changamoto katika jamii ya watanzania na duniani kwa ujumla.

Hayo yamebainishwa na Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma, Prof Davis Mwamfupe, alipokuwa akifungua warsha ya Watafiti kutoka nchi ya Kenya, Afrika Kusini, Rwanda, Uganda na wenyeji Tanzania, uliofanyika katika Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP) jijini Dodoma.

Mtahiki Meya Mwamfupe, alisema kuwa ili utafiti uwe na thamani nilazima kutumia mbinu zinazoaminika bila kujali utafiti unaofanyika unahusu kitu gani, kwa lengo la kuondoa mkanganyiko wa matokeo hivyo kuwa na tija kwa jamii.

“Utafiti wa kisayansi ni ule unaotumia njia zinazokubalika kimataifa na kuwa na uwezo wa kukabiliana na changamoto zikiwemo za kutokuwa na usawa hasa katika pande mbili za Dunia yani Kasikazini na Kusini lakini pia katika jamii moja na nyingine”, alieleza Meya Prof. Mwamfupe.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Prof. Adolf Mkenda, ambaye alikua mtoa mada katika warsha hiyo alisema kuwa, katika wasilisho lake wadau kutoka nje ya nchi wamefurahishwa na uchambuzi kuhusu hali ya uchumi ambapo ilielezwa namna watu wenye kipato kikubwa kupenda kununua bidhaa nje jambo ambalo limeifanya Serikali ya Tanzania kuweka mikakati ya kutatua tatizo hilo ili kujenga uchumi wa bnchi.

Alisema kuwa tabia ya wenye kipato kikubwa kununua bidhaa nje kuna kosesha ajira, hivyo Serikali imeamua kuweka mikakati ya Ujenzi wa uchumi katika Nyanja ya viwanda, kilimo na miundombinu ikiwemo ya umeme, jambo ambalo ni ajenda ya Afrika

Kwa upande wake Mratibu wa Warsha hiyo ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo Cha Mipango Vijijini, Dkt. George Kanyasi, alisema kuwa lengo la Warsha hiyo ni kuwakutanisha watafiti wanaochipukia na wanasayansi kutoka nchi tano za Afrika kwa lengo la kuwajengea uwezo ili kupata watafiti mahiri.

Amesema kuwa kazi ya tafiti sio tu kuongeza maarifa lakini pia kutatua changamoto katika maeneo yaliyokosa usawa katika elimu, uchumi, siasa na masuala ya kijamii

Mkutano huo pamoja na kuwashirikisha watafiti kutoka nje ya nchi, pia umewahusisha baadhi ya wadau kutoka Halmashauri ili kujua changamoto zao na kuweka mikakati ya kuzitatua, aidha warsha zinazofuata zitawakutanisha Wakurugenzi wa Halmashauri na Maafisa Mipango ili waweze kubaini matatizo ya maeneo yao na waweze kuyatatua.

Mwisho


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527