Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesema serikali yake tayari imenunua mtambo wa kujikinga na makombora kutoka Urusi.
Erdogan amewaambia wanachama wa chama chake cha AKP kuwa mfumo huo wa kujikinga na makombora utawasili Uturuki mwezi Julai mwaka huu.
Mpango huo wa Uturuki kununua mtambo huo kutoka Urusi umekuwa kiini cha mvutano na muungano wa kujihami wa NATO, ambao Marekani na Uturuki ni wanachama.
Marekani na washirika wengine wa NATO wanahofia kuwa Urusi huenda ikazipeleleza ndege za NATO kwa kutumia mtambo huo wa S-400.
Ili kuizuia Uturuki kufanya ununuzi huo, Marekani ilisitisha mpango wa pamoja wa ndege za kivita aina ya F-35 na kuitishia Uturuki na vikwazo zaidi vya kiuchumi.