TCRA : NAMBA ZA SIMU AMBAZO HAZITASAJILIWA KWA ALAMA ZA VIDOLE ZITAFUNGWA

Mkuu wa TCRA Kanda ya Ziwa,Mhandisi Francis Mihayo akizungumza katika mkutano wa wadau wa mawasiliano kanda ya ziwa leo - Picha na Kadama Malunde - Malunde1 blog

Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Kanda ya Ziwa,Mhandisi Francis Mihayo amesema laini za simu ambazo hazitasajiliwa baada ya Desemba 31,2019 zitafungwa.


Mhandisi Mihayo amesema hayo leo Alhamis Juni 13,2019 wakati wa mkutano wa wadau wa sekta ya mawasiliano Kanda ya Ziwa kuhusu kupokea maoni,mapendekezo na kusikiliza kero zinazohusu utendaji wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)uliofanyika katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa mkoa jijini Mwanza.

"TCRA inaendelea kusimamia sekta ya mawasiliano kwa karibu ,Tumeanzisha usajili mpya wa namba za simu kwa kutumia alama za vidole,mfumo unajulikana kama 'Biometria' ambapo zoezi hili lina nia njema ya kuhakikisha linaondoa kabisa uhalifu kupitia mitandao ya simu.Zoezi hili limepangwa kufikia kikomo ifikapo Desemba 31,2019,tunaamini kuwa pindi tutakapomaliza hili zoezi haya matatizo ya udanganyifu/utapeli mitandaoni yatakwisha",alisema Mhandisi Mihayo.

"Naomba kuwakumbusha kufanya usajili sasa na kama hauna kitambulisho cha taifa basi hakikisha unafanya utaratibu wa kutafuta kitambulisho kutoka Mamlaka ya Vitambulisho NIDA na kamwe usisubiri muda wa mwisho uliowekwa ufike ili kuepuka usumbufu wowote utakaotokea",aliongeza .

Alisema idadi ya laini zinazotakiwa kusajiliwa ni moja kila mtandao kama unahitaji zaidi ya moja unatakiwa utoe maelezo unazihitaji kwa matumizi yapi huku akisisitiza kuwa hakuna kitambulisho kingine zaidi ya NIDA kitakachotumika kwenye usajili wa kutumia alama za vidole.

Mkutano wa wadau wa sekta ya mawasiliano Kanda ya Ziwa umekutanisha pamoja viongozi wa dini kutoka kamati ya amani mkoa wa Mwanza,viongozi wa baraza la watumiaji wa bidhaa za Mawasiliano (TCRA CCC),jeshi la polisi mkoa wa Mwanza kitengo cha makosa ya mitandaoni,makampuni yanayotoa huduma za mitandao ya simu na intaneti,mafundi simu,vituo vya utangazaji vya Televisheni na Redio,waagizaji,wasambazaji na wauzaji wa vifaa vya mawasiliano,watoa huduma wa visimbuzi vya STARTIMES & Basic Transmission na watoa huduma wa maudhui mtandaoni. 
Mkuu wa TCRA Kanda ya Ziwa,Mhandisi Francis Mihayo akizungumza katika mkutano wa wadau wa mawasiliano kanda ya ziwa 
Soma pia : Picha : TCRA YAKUTANA NA WADAU WA MAWASILIANO KANDA YA ZIWA

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527