Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.
Serikali imelieleza bunge kuwa wenyeviti wa vijiji ,mitaa na vitongoji siyo watumishi wa umma na hivyo hawaajiriwi na kulipwa mishahara kama ilivyo watendaji wa mitaa na vijiji.
Hayo yamesemwa leo Juni 13,2019 bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais TAMISEMI Mwita Waitara wakati akijibu Swali la mbunge wa Mtwara mjini,Muftaha Nachuma aliyehoji ,wenyeviti wa serikali za vijiji na vitongoji wanafanya kazi kubwa na ngumu sana,je,serikali haioni umuhimu wa kuwalipa mishahara kama ilivyo kwa watendaji wa vijiji.
Akijibu Swali hilo,Mhe.Waitara amesema serikali inatambua kazi kubwa na nzuri inayofanywa na wenyeviti wa vijiji ,mitaa na vitongoji katika shughuli za maendeleo na kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi wa wenyeviti wa serikali za vijiji ,mitaa,vitongoji na wajumbe wa serikali za mitaa za mwaka 2014 zilizotolewa kupitia tangazo la serikali Na.322 na Na.323,sifa zinazomwezesha mkazi wa mtaa ,kijiji na kitongoji kuchaguliwa kuwa mwenyekiti au mjumbe wa serikali za mitaa ni pamoja kuwa na shughuli halali inayomwingizia kipato.
Aidha ,Naibu Waziri Mwita Waitara amesema wenyeviti wa vijiji,mitaa,na vitongoji sio watumishi wa umma na hivyo hawaajiriwi na kulipwa mishahara kama ilivyo kwa watendaji wa vijiji na mitaa.
IHata hivyo,Mhe.Waitara amesema kutokana na kazi ngumu wanazofanya ,serikali inawalipa posho kutokana na asilimia 20% ya mapato ya ndani ya Halmashauri kwa mujibu wa sheria ya fedha za serikali za mitaa ,Sura 290 na ulipaji wa posho wa viongozi hao unategemea na makusanyo ya Halmashauri.