MAMLAKA YA CHAKULA NA DAWA (TFDA) YAFUNGUA OFISI YA KANDA MPYA YA ZIWA MASHARIKI SIMIYU

Na Stella Kalinga, Simiyu

Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) imefungua rasmi Ofisi ya Kanda mpya ya Ziwa Mashariki itakayohudumia mikoa ya Simiyu, Mara na Shinyanga ambapo makao makuu ya kanda hiyo yatakuwa Mjini Bariadi mkoani Simiyu.

Akitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka, Kaimu Meneja wa TFDA Kanda ya Ziwa Mashariki, Bi. Nuru Mwasulama amesema mamlaka hiyo imeanzisha Kanda Mpya ya Ziwa Mashariki inayojumuisha mikoa ya Simiyu, Mara na Shinyanga ili kusogeza huduma kwa wananchi na kuharakisha ukuaji wa uchumi wa kati unaotegemea viwanda.

Amesema ofisi hii itajishughulisha na usajili wa maeneo yanayo jihusisha na uzalishaji na uuzaji wa chakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba, kupokea maombi ya usajili wa bidhaa za vyakula vinavyofungashwa, kufanya ukaguzi wa bidhaa za vyakula katika soko kuwalinda walaji na  kudhibiti usindikaji wa chakula dawa na vipodozi.

Kazi nyingine zitakazofanywa na kanda hii ni kutoa vibali vya uingizaji nchini na usafirishaji wa chakula nje ya nchi, kufanya ufuatiliaji wa bidhaa za vyakula katika soko, kuhamasisha matumizi sahihi ya dawa, vipodozi na vifaa tiba pamoja na kuelimisha na kutoa taarifa kwa wadau na wananchi kwa ujumla kuhusu bidhaa zinazothibitiwa na mamlaka.

Aidha, Mwasulama amesema Ofisi ya kanda hii itatekeleza majukumu yake kwa kushirikiana na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, ambapo wataalam waliopo kwenye wilaya, manispaa, miji na majiji watasimamia sheria ya chakula na dawa kwa mujibu wa kanuni ya kukasimu baadhi ya majukumu na madaraka ya TFDA katika  Halmashauri.

Akizungumza na baadhi ya wataalam wa Mkoa wa Simiyu na TFDA katika ufunguzi huo, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema ni vema Taasisi nyingine zinazohitajika katika uwekezaji wa viwanda na maeneo mengine ya uwekezaji zikaiga mfano wa TFDA  kwa kusogeza huduma karibu na wananchi ili waweze kupata huduma kwa wakati.

“Hiki kilichofanywa na TFDA ni vizuri taasisi nyingine nazo ziige, kama leo TFDA ipo Simiyu kama Kanda ya Ziwa Mashariki ningetamani kuwaona TBS, NEMC, OSHA wako Simiyu kama Kanda ya Ziwa Mashariki na Taasisi zote ambazo kwenye uwekezaji wa viwanda na maeneo mengine ya uwekezaji zinakuwa karibu na maeneo ya kutolea huduma” alisisitiza Mtaka.

Katika hatua nyingine Mtaka ametoa wito kwa watumishi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa wanaotekeleza majukumu waliyokasimiwa na TFDA kufanya majukumu hayo kwa mujibu sheria huku akiwaasa  kuacha tabia ya kufungia biashara za wananchi bila kuwaelimisha badala yake wawasaidie kuwapa elimu ili wazalishe bidhaa bora kwa walaji.

Naye Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi, Dkt. Mike Mabimbi akizungumza kwa niaba ya waganga wakuu wa wilaya ambao ni Makatibu wa kamati za ukaguzi wa chakula na dawa amesema watahakikisha wanasimamia utekelezaji wa majukumu wanayokasimiwa  na TFDA kwa mujibu wa sheria na akashukuru TFDA kusogeza huduma karibu na wananchi.

MWISHO


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527