PINDA: MNAPASWA KUDUMISHA NIDHAMU YA MATUMIZI YA FEDHA BAADA YA KUSTAAFU

NA. MWANDISHI  WETU
Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Mizengo  Pinda amewaasa watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu wanaotarajia kustaafu hivi karibuni kudumisha nidhamu katika matumizi ya fedha baada ya kustaafu utumishi wa umma na kujikita katika shughuli za uzalishaji.


Akizungumza katika makazi yake yaliyopo Zuzu Jijini Dodoma  wakati watumishi hao walipomtembelea Juni 20, 2019 kwa lengo la kujifunza shughuli mbalimbali za uzalishaji katika sekta ya kilimo na mifugo ikiwa ni sehemu ya  maandalizi ya kustaafu pamoja na kuadhimisha wiki ya Utumishi wa Umma , Mhe Pinda amesema kuwa kuna umuhimu mkubwa kwa watumishi wote wanaotarajia kustaafu kujenga utamaduni wa nidhamu katika matumizi ya rasilimali ikiwemo fedha watakazopata kama kiinua mgongo.

" Nidhamu ya maisha baada ya kustaafu ni muhimu sana hivyo niwaase mjitahidi kuacha baadhi ya masuala ambayo mnafanya  kwa sasa kama starehe na mambo yote yanayoendana na kupoteza muda wenu badala yake mjikite katika uzalishaji" Alisisitiza Mhe. Pinda

Aliongezea kuwa  ni vyema watumishi  hao wakajenga utamaduni wa kufanya kazi za uzalishaji na kujikita katika usimamizi wa  miradi ya uzalishaji watakayoanzisha kwa lengo la  kujiongezea kipato na kukuza uchumi .

Pia aliwaasa watumishi hao kuzingatia mawazo kutoka kwa watumishi ambao wameshastaafu na wamefanikiwa  kimaisha baada ya kustaafu.

"Kila mmoja wenu akatekeleze miradi ya kujikwamua kiuchumi kwa kuzingatia mafao atakayopata badala ya kutaka kufanya mambo kwa mashindano bali kila mtu ajikune kulingana na mkono wake unapoweza"

Kwa upande wake Katibu mkuu wa  Ofisi ya Waziri Mkuu  (Bunge na Waziri Mkuu) Bi Maimuna Tarishi amesema kuwa mafunzo yakuwajengea uwezo wa kujiandaa  kustaafu,  yameandaliwa ikiwa ni sehemu ya  maadhimisho ya wiki ya utumishi wa umma.

Aliongeza kuwa watumishi hao wamefarijika kuona shughuli za uzalishaji anazofanya Waziri Mkuu mstaafu Mhe. Mizengo Pinda na kuwa ni mfano kwa watumishi wa umma wanaostaafu  na kuanza kujikita katika uzalishaji mali .

Ofisi ya Waziri Mkuu imeandaa mafunzo ya siku 5 kwa watumishi wake wanaotarajia kustaafu ili kuwapa mbinu za kisasa zinazolenga kuwawezesha kuendelea na maisha yao baada ya kustaafu huku wakiendeleza shughuli za uzalishaji  zitakazowawezesha kuendesha maisha yao ya kila siku na kuweza kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza baada ya kustaafu.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527