LUGOLA: HAKUNA TISHIO LOLOTE LA UGAIDI NCHINI

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amesema Watanzania wasiwe na hofu juu ya tishio la ugaidi kwani nchi ina usalama wa hali ya juu.


Akizungumza leo Juni 20, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wakimbizi Duniani, amesema vyombo vya ulinzi vinaendelea na uchunguzi juu ya suala hilo.

“Serikali iko imara na vyombo vya ulinzi na usalama viko imara vimejipanga vizuri kwa jambo au tishio lolote la usalama.

“Tahadhari ambayo imetolewa na wenzetu wa Marekani hizi ni sehemu ya taarifa za kawaida na tumeweza kuwasiliana nao kupitia jeshi la polisi.

“Watanzania wasiwe na hofu wala wasiwasi nchi iko imara  ina usalama wa hali ya juu na vyombo vinaendelea kufanya kazi yake,” amesema Lugola.


Awali, Mwakilishi wa UNHCR nchini Tanzania, Chansa Kapaya anasema siku ya wakimbizi inatoa nafasi ya kutafakari na kukumbuka kwamba wakimbizi ni watu na wanatamani nchi zao ziwe na amani waweze kurejea.

"Tunaunga mkono Serikali ya Tanzania katika kutoa huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na chakula, mavazi, maji safi na makazi," amesema.

Mpaka Mei 2019 Tanzania ilikuwa inahifadhi wakimbizi 312,152 wengi wao walitokea Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Jana Jumatano Juni 19, 2019 Ubalozi huo ulieleza kuwapo kwa uvumi wa kutokea kwa shambulio la kigaidi katika eneo la Masaki hususan hoteli za kitalii na maduka ya maeneo hayo ya ufukwe wa Bahari ya Hindi.

Ubalozi huo uliwataka wakazi kuwa makini na maeneo hayo, kujiepusha na makundi na kufuatilia taarifa kupitia vyombo vya habari.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post