RUGEMALIRA AJARIBU TENA BAHATI YAKE YA KUPEWA DHAMANA MAHAKAMA YA RUFAA


Mshtakiwa wa kesi ya uchotaji fedha katika Akaunti ya Tegeta Escrow, James Rugemalira kwa mara  nyingine tena amejaribu bahati yake ya kupata dhamana katikati ya mashtaka yasiyo na dhamana yanayomkabili yeye na mwenzake, baada ya kuiomba Mahakama ya Rufani nchini Tanzania imwachie huru kwa dhamana.

Rugemalira ambaye anakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi  yenye mashtaka ya utakatishaji fedha ambayo hayana dhamana, ametoa maombi hayo  Jumatano Juni 19, 2019, wakati wa usikilizwaji wa rufaa yake.

Katika rufaa hiyo Rugemalira anapinga uamuzi wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, (Mahakama ya Ufisadi) kumnyima dhamana, uliotolewa na aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahaka hiyo Firmin Matogolo, Agosti 30, 2019.

Rufaa hiyo imesikilizwa jana na  jopo la majaji watatu, Richard Mziray (kiongozi), Winfrida Korosso na Ignas Kitusi, ambapo Rugemalira licha ya kuwa na mawakili wawili, ameomba na akaruhusiwa kutoa hoja zake za rufaa yeye mwenyewe, kabla ya mawakili wake.

Baada ya kusikiliza hoja hizo, Jaji Mziray ameahirisha shauri hilo hadi tarehe nyingine itakayopangwa na Msajili wa Mahakama ya Rufani kwa ajili ya uamuzi.

Rugemalira licha ya kukabiliwa na mashtaka hayo ambayo hayana dhamana alikimbilia mahakamani hapo kuomba afutiwe mashtaka ya utakatishaji fedha kisha aachiwe huru kwa dhamana kwa madai hati ya mashtaka yanayowakabili ina kasoro za kisheria, kwa kutokuwa na  maelezo yanayoonyesha kosa la utakatishaji fedha.

Hata hivyo  Jaji Matogolo alitupilia mbali maombi hayo akisema Mahakama hiyo haina mamlaka ya kumpa nafuu alizokuwa akiziomba.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527