ASKARI ATAKAYEKAMATA BODABODA NA KUPELEKA KITUONI NJE YA MAKOSA MATATU YANAYOTAMBULIKA KUKIONA CHA MOTO

Na Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.
Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi,Kangi Lugola amewataka askari kote nchini kuacha tabia ya kukamata ovyo waendesha bodaboda na kuziweka kizuizini pikipiki zao katika vituo vya polisi bila sababu na makosa ya Msingi.

 
Waziri Lugola amesema hayo  Juni 17,2019 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu  maswali mbalimbali ya  yaliyoelekezwa katika Wizara yake ambapo  wamedai pamekuwepo na changamoto ya baadhi ya askari wa vikosi vya usalama barabarani kuonekana kuwa kero kwa waendesha bodaboda kutokana na kukamata pikipiki  na kuziweka kizuizini kwa muda mrefu  licha ya makosa hayo kuwa na uwezekano wa kutatulika  kwa utaratibu maalum.

Akijibu Maswali hayo,Waziri Lugola amesema pikipiki inaweza ikakamatwa na kuwekwa kizuizini katika kituo cha polisi kwa makosa matatu  ambayo ni endapo imehusika kwenye uhalifu,imeokotwa  na haina mwenyewe  na sababu  ya tatu imesababisha ajali kinyume na hapo hairuhusiwi  kukamatwa na kupelekwa kituoni.

Aidha,Waziri Lugola amesema ajali za barabarani zimekuwa zikitokea mara kwa mara hapa nchini ,hivyo watanzania       wanatakiwa kufuatilia bima pindi wanapopata ajali.

Awali  akijibu Swali  la Msingi la Subira Mwaifunga,Mbunge wa viti Maalum,lililohoji juu ya tishio la ajali za barabarani,Naibu Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi Mhandisi Hamad Masauni  amesema   serikali ina mkakati madhubuti ya kupambana na tatizo hilo ikiwa ni pamoja kuongeza wigo wa elimu kwa njia ya redio ,luninga na machapisho ya vipeperushi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527