TUME YA MADINI YATOA LESENI ZA MADINI 832 NDANI YA MIEZI MITATU

Na Greyson Mwase, Dodoma

Mkurugenzi wa Huduma za Leseni na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) wa Tume ya Madini, Mhandisi, Yahya Samamba amesema kuwa kati ya kipindi cha mwezi Januari, 2019 na Machi, 2019, Tume ya Madini imepitisha maombi ya leseni za madini 832 kati ya maombi 951 yaliyowasilishwa.

Mhandisi Samamba ameyasema hayo kwenye kikao cha Kamati ya Ufundi ya Tume ya Madini kilichofanyika mapema leo tarehe 13 Mei, 2019 jijini Dodoma chenye lengo la kupokea na kujadili taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Tume ya Madini katika kipindi cha mwezi Januari, 2019 hadi Machi, 2019.

Kikao hicho kilishirikisha Makamishna wa Tume ya Madini, Profesa Abdulkarim Mruma na Dk. Athanas Macheyeki, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Tume, William Mtinya, Mkurugenzi wa Ukaguzi na Biashara ya Madini, Dk. Venance Mwase pamoja na mameneja na watendaji kutoka Tume ya Madini.

Alifafanua kuwa awali Idara yake ilipokea na kushughulikia  maombi mapya ya leseni za madini  951 ikiwa ni pamoja na maombi ya leseni za utafutaji wa madini 77, maombi ya leseni za uchimbaji mdogo wa madini 728 na maombi ya leseni za uchenjuaji wa madini 15.

Maombi mengine yaliyopokelewa ni pamoja na maombi ya leseni za biashara ya madini 131 ambapo yalihakikiwa  kama yamekidhi matakwa ya Sheria ya Madini na Kanuni zake.

Alisisitiza kuwa mara baada ya zoezi la uchambuzi kukamilika  maombi ya leseni za madini 832 yalipitishwa na kusisitiza kuwa bado Tume ya Madini inaendelea kupokea maombi ya leseni mbalimbali za madini na kuyafanyia kazi.

Akizungumzia mafanikio katika sekta ya madini kwa ujumla, Mhandisi Samamba alisema kuwa Serikali imeboresha Sheria ya Madini pamoja na kanuni zake inayomtambua mzawa kama mmiliki wa madini na kuwataka wananchi hususan wachimbaji wadogo kuchangamkia fursa mbalimbali.

Katika hatua nyingine Mhandisi Samamba aliwataka wachimbaji wadogo wa madini wasio rasmi kuunda vikundi na kuomba leseni za madini na kusisitiza kuwa Tume ya Madini kupitia Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa ipo tayari kuwasaidia.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post