WAZEE WASHAURI WA MAHAKAMA WATOA YA MOYONI KUHUSU MAUAJI YA MWANAFUNZI WA SCOLASTICA


Wazee washauri wa mahakama katika kesi ya mauaji ya mwanafunzi wa shule ya Scolastica, Humphrey Makundi (16), wametofautiana huku mmoja akisema washtakiwa wote wana hatia ya mauaji ya kukusudia.

Hata hivyo, mmoja wa wazee hao ameona mshtakiwa wa pili, Edward Shayo ambaye ni mmiliki wa shule hiyo apewe adhabu ndogo kwa maelezo kuwa kosa lake ni kuzembea kutoa taarifa ya mauaji.

Kifungu cha 196 cha kanuni ya adhabu sura ya 16, kinaeleza mtu yeyote anayesababisha kifo cha mtu mwingine bila uhalali wa kisheria anatenda kosa la mauaji na adhabu yake ni kunyongwa hadi kufa.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni mshtakiwa namba moja, Hamis Chacha ambaye ni mlinzi wa shule na Laban Nabiswa, mshitakiwa wa tatu ambaye ni mwalimu wa nidhamu shuleni hapo.

Kauli za wazee hao zilijitokeza juzi kati ya saa 11:00 alasiri na saa 1:30 usiku wakati Mahakama Kuu chini ya Jaji Firmin Matogolo anayesikiliza kesi hiyo, ilipoketi kupokea maoni ya wazee hao.

Kabla ya kuanza kupokea maoni hayo, Jaji Matogolo aliwasomea wazee hao muhtasari wa ushahidi wa upande wa mashtaka na ule wa utetezi wa washtakiwa pamoja na mashahidi wao waliowaita.

“Nyie (wazee washauri) ni waamuzi wa ushahidi siyo waamuzi wa sheria. Ili kuthibitisha shtaka la mauaji ya kukusudia ni lazima kuwe na kitendo cha kuua na dhamira ya kuua,” alisema Jaji Matogolo.

“Dhamira ya kuua inaweza kuthibitishwa na aina ya silaha iliyotumika kama ipo na nguvu iliyotumika. Mambo mengine ni matendo ya mshtakiwa kabla, siku ya mauaji na baada.”

Jaji alisema, “mmesikia mazingira yote ya kupotea kwa mwanafunzi (Humphrey) na baadaye mwili wake kupatikana mtoni na kutambuliwa kwake. Pia mmesikia sababu za kifo kuwa ni kuumia sana kichwani.

“Naamini pia mlisikia ushahidi wa shahidi wa 14 (Irene Mushi) wa upande wa mashtaka ambaye ni mlinzi wa amani kitu ambacho ndicho kitovu na ubishani mkubwa wa tukio hili.” Shahidi huyo ndiye aliyeandika maelezo ya ungamo ya mshtakiwa Chacha, akidaiwa kueleza hatua kwa hatua namna alivyomua mwanafunzi huyo na baadaye kuwashirikisha Nabiswa na Shayo.

Jaji Matogolo alisema katika mashauri ya mauaji mshtakiwa anaweza kuwa na utetezi na unaweza kuegemea katika ulevi, ukichaa au bahati mbaya na sababu nyingine.

“Lakini Utetezi huo haumuondolei kabisa mshtakiwa kosa la mauaji ya kukusudia, bali linampunguzia tu kutoka kuwa kosa la mauaji ya kukusudia na kuwa kosa la kuua bila kukusudia,”alifafanua jaji huyo.

“Vilevile mliweza kuwapima washtakiwa nani anasema ukweli na nani hasemi ukweli. Katika kesi hii imeegemea ushahidi wa mazingira kwa vile hakuna shahidi aliyeshuhudia mauaji hayo.”

Hata hivyo, Jaji Matogolo alisema ushahidi wa mazingira unakubalika pia kutokana na muunganiko wa ushahidi, hivyo ni wajibu wa wazee hao kupima mambo hayo wakati wanatoa maoni yao.

Baada ya maelezo hayo, mzee wa kwanza, Focus Mrema alisema amesikiliza kesi hiyo na mashahidi kwa umakini mkubwa, na kwamba hakuna ubishi kuwa kifo cha mwanafuzni huyo kilitokana na kuuawa.

Mzee huyo alieleza kwa maoni yake, upande wa Jamhuri umeweza kuthibitisha shtaka dhidi ya washtakiwa wote na akaiomba mahakama iwatie hatiani na iwape adhabu kwa mujibu wa sheria.

Kwa upande wake, mzee wa pili, Fatuma Ndutu, alisema baada ya kusikiliza ushahidi uliotolewa ana maoni kuwa mshtakiwa namba moja (Chacha) ana hatia kwa sababu alikiri kwenye ungamo lake.

Hata hivyo, alisema ana maoni kuwa ushiriki wa mshtakiwa namba mbili (Shayo) na namba tatu (Nabiswa) ni kwa kupitia mshtakiwa wa kwanza, hivyo wao wanaweza kupunguziwa adhabu.

“Jamhuri wamethibitisha shtaka kwa mshtakiwa wa kwanza bila kuacha mashaka, hivyo ana hatia kutokana na kukiri kwake. Mahakama itoe adhabu kwa mujibu wa sheria kwa kila mshtakiwa,” alisema.

Naye Khalfan Abrahaman alisema anaona kuwa upande wa mashtaka umeweza kuthibitisha shtaka la mauaji ya kukusudia dhidi ya mshtakiwa Chacha na Nabiswa.

“Kwa kitendo walichokifanya washtakiwa cha kushiriki kutupa mwili wa mtoto Mto Ghona ni kitendo cha kinyama na huwezi kutupa au kuhamisha mtu aliyekufa bila kuhusika na kifo chake,” alisema.

“Hivyo naiomba mahakama iwaone mshtakiwa wa kwanza na wa tatu wana hatia ya mauaji ya kukusudia. Hao wawili ni wahusika wakuu waliosababisha kifo cha mwanafunzi.”

Alisema, “vilevile pamoja na mshtakiwa wa pili (Shayo) yeye apewe adhabu kutokana na kuzembea ku-report (kutoa taarifa ya mauaji) aliyoipata kutoka kwa mshtakiwa wa kwanza.

Baada ya kumaliza kutoa maoni yao, Jaji Matogolo aliwaeleza wazee hao kuwa kwa kawaida hafungwi na maoni yao, bali anaweza kuyatumia au asiyatumie wakati anafanya uamuzi wa kesi hiyo.

“Kama nilivyosema nyinyi ni waamuzi wa ushahidi na mimi sasa nakwenda mbele zaidi kuangalia sheria inasemaje. Tarehe ya hukumu mtajulishwa na msajili. Hukumu haitachukua muda,” alisema.

Mwanafunzi huyo anadaiwa kuuawa Novemba 6, 2017 na mwili wake kutupwa Mto Ghona uliopo mita 300 kutoka ilipo shule ilipo na baadaye ukazikwa na Manispaa ya Moshi kwa kuwa haukutambuliwa.

Baadaye polisi kupitia Divisheni ya Mashtaka ya Taifa (NPS) waliomba kibali cha kufukuliwa kwa mwili huo na baba mzazi, Jackson Makundi aliutambia na baadaye kuthibitishwa na vinasada (DNA).

Katika kesi hiyo, upande wa mashtaka uliwajumuisha mawakili wanne huku washtakiwa wakitetewa na jopo la idadi kama hiyo ya mawakili.

Credit: Mwananchi


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527