MKE,HAWARA MTOTO WAUA MUME MOROGORO

Boniface Agustino (46) mkazi wa Chamwino Manispaa ya Morogoro, anadaiwa kuuawa na mke, mpenzi wake na mtoto wake kwa kupigwa kwa kitu kizito kichwani kwa kile kinachodaiwa kuwa wivu wa kimapenzi.


Majirani walioshuhudia tukio hilo, akiwamo Mariam Mohamed, walidai kuwa juzi majira ya saa 8:00 mchana, walisikia vishindo na kelele kutoka kwa mwanamume huyo akiomba msaada na kudai kuwa mke wake anataka kumuua huku wakiwa chumbani kwao.

Mohamed alisema, awali mwanaume huyo alikuwa na ugomvi na mke wake, jambo ambalo lilisababisha ndugu kulisuluhisha, lakini wanashangazwa kuona mwanamke huyo akishirikiana na mtoto wake, wamefikia hatua ya kufanya mauaji hayo.

Alidai kuwa mwanamke huyo, Neema Godfrey, alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanamume aliyefahamika kwa jina moja la Salum ambaye alikuwa mpangaji wake katika nyumba waliyokuwa wakiishi na mume wake, huku pia mwanamume huyo akiwa na uhusiano wa kimapenzi na binti yake, Alphonsina Boniface.

Pia Nipashe ilizungumza na ndugu wa marehemu, Revina Makundi, ambaye alisema kaka yake huyo na mkewe walikuwa na ugomvi kila mara ambao yeye alikuwa akiusuluhisha kuhusu Boniface kumbaka binti yake wakati akiwa mdogo kwa imani za kishirikina.

Aidha, Makundi alisema wanandoa hao walikuwa na ugomvi wa kimapenzi baada ya mpangaji wao kutembea na Godfrey na binti yake, hatua iliyosababisha mpangaji huyo kufukuzwa, lakini baadaye alirudi.

Mtendaji wa Kata ya Chamwino, Bright Sospeter, alisema majira ya 10:00 jioni alisikia watu wakieleza tukio hilo huku wakiwa na hisia za kutokea mauaji ndipo walijumuika na viongozi wengine.

Alisema walipofika eneo la tukio walimhoji mwanamke ambaye ni mke wa marehemu na kusema mumewe alirukwa na akili mchana na ndiyo maana alisema anauawa na muda huo wakati anaulizwa hakuwapo.

Sospeter alisema walipoingia ndani, walimkuta na kumkuta binti na kumuuliza ndipo akasema baba yake alienda kwa Ustaadhi kuombewa, hivyo hayupo jambo lililowafanya walazimike kupekua nyumba nzima na ndipo walipokuta akiwa tayari amefariki dunia akiwa chooni, huku pembeni yake kukiwa na mchi na damu sakafuni.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Wilbroad Mutafungwa, alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo na kusema wanawashikilia watu watatu kwa mahojiano zaidi.

Aliwataja watu hao kuwa ni Neema Godfrey (41) mkazi wa Chamwino, Alponcina Boniface (19) na mtu mwingine ambaye hakumtaja kwa sababu za kiuchunguzi.

Mutafungwa alisema inadaiwa kuwa mpangaji aliyekuwa amehamishwa alihusika baada ya kuingia ndani akiwa amevaa vazi aina ya dela hadi usoni na baadaye kutoroka. Aliwataka wananchi wa mkoa wa Morogoro hususan wakazi wa Chamwino, kushirikiana na polisi kufanikisha mtuhumiwa mwingine wa mauaji kupatikana.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post