WATU 121 WAPOTEZA MAISHA KATIKA MACHAFUKO LIBYA


Watu 121 wamepoteza maisha katika mapigano baina ya makundi ya wanamgambo hasimu yanayopambana kuchukua udhibiti wa mji mkuu wa Libya, Tripoli.

Shirika la afya duniani WHO, limesema katika taarifa yake kwamba watu wengine 561 wamejeruhiwa tangu kamanda Khalifa Haftar alipoanzisha mashambulizi mapema mwezi huu kuudhibiti mji wa Tripoli, ambao hivi sasa uko mikononi mwa serikali inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.

Katika taarifa yake ya awali kupitia mtandao wa kijamii wa twita, shirika hilo limekemea mashambulizi ya kila mara dhidi ya wafanyakazi wa afya na magari wakati wa mapigano hayo yaliyoanza Aprili 5. Mapema wiki hii shirika hilo la Umoja wa Mataifa lilisema takribani watu 8000 wameyakimbia makazi yao nchini humo.

Rais wa Misri Abdel-Fattah el-Sisi alikutana na Kamanda Haftar mjini Cairo kufanya majadiliano juu ya mashambulizi wakati kukiwa na ongezeko la shinikizo la kimataifa kukomesha mashambulizi. Misri na Ufaransa zimeendeleza uhusiano na kamanda Haftar.

Serikali ya Libya inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa imesema kuwa vikosi vyake vimeitungua ndege ya kivita inayomilikiwa na Haftar kusini mwa mji mkuu wa Tripoli. Chanzo kutoka ndani ya jeshi la taifa la Libya la kamanda Haftar LNA, kimethibitisha kutunguliwa kwa ndege ya MIG-23 lakini kikisema ni kwa sababu za kiufundi.

Taarifa zaidi zinasema rubani wa ndege hiyo alifanikiwa kutoka salama na kukataa ripoti kuwa amekamatwa na serikali ya Libya inayotambulika na Umoja wa Mataifa.

Jeshi la LNA lilianzisha mashambulizi siku 10 zilizopita ili kuchukua udhibiti wa mji mkuu, Tripoli ambako ndipo ilipo serikali ya Umoja wa Kitaifa GNA inayoongozwa na Fayez al-Sarraj. Msemaji wa serikali ya Libya Mohanad Yuns alisema mwishoni mwa juma kuwa wanakaribisha usitishaji mapigano.

"Serikali ya Umoja wa kitaifa inakaribisha usitishaji mapigano, lakini haimaniishi kwamba inakubaliana na kuendelea kwa hali ya sasa. Vikosi vya uvamizi ni lazima virudi vilikotoka mara moja".

Kwa ujumla pande zote mbili zimekuwa zikifanya mashambulizi ya ardhini na angani na kutupiana lawama kwa kuwalenga raia.

-DW


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post