SUALA LA WAFUNGWA WAJAWAZITO LAZUA GUMZO BUNGENI

Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.

Serikali imesema itaendelea kuwajali wanawake , wafungwa wajawazito kwa kuwapatia huduma zote  anazopaswa kupatiwa mama mjamzito.

Hayo yamesemwa  April 17 bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Mambo ya ndani ya nchi Mhe.Kangi Lugola wakati akijibu swali la mbunge wa viti maalum mhe.Angelina Adam Malembeka aliyehoji ,baadhi ya akina mama wajawazito huingia gerezani  wakiwa wajawazito na kujifungulia gerezani  je,ni huduma gani hupata ili kuhakikisha anajifungua salama.

Katika majibu yake Mhe.Lugola amesema jeshi la Magereza limekuwa likitoa huduma za afya ,chanjo na kuhakikisha wanahudhuria kliniki ya akina mama wajawazito katika vituo vya afya vya magereza.

Aidha amesema jeshi la magereza limekuwa likiwapatia wafungwa wajawazito vyakula vinavyohitajika kiafya kwa kuzingatia maelekezo  na ushauri wa madaktari wa  Magereza.

Katika swali lake la nyongeza Mhe.Malembeka   amehoji ,Serikali inawasaidiaje watoto wanaozaliwa magerezani kisaiklojia  na kielimu na kwanini pasiruhusiwe vifungo vya nje  kwa akina mama wajawazito na wenye watoto ili waweze kulea watoto wao vizuri.

Akijibu Swali hilo,mhe.Lugola amesema kuna utaratibu watoto wanaozaliwa Magerezani  wamekuwa wakisoma shule za awali zilizoko magerezani  na wanawake wafungwa wenye vifungo  chini ya miaka mitatu kuna sheria ya “Probation for Offender  “pamoja na sheria ya “Community Services “ ambapo pia huwa na utaratibu wa kuwaondoa wafungwa wajawazito na wenye watoto  ili wawe na vifungo mbadala.

Hata hivyo watoto wanaoishi Magerezani wanapokuwa wakubwa na kufikia umri wa kuishi bila mama zao ,ndugu zao wamekuwa wakishirikishwa ili waweze  kutoa malezi kwa watoto ambao mama zao wako magerezani.

Katika hatua nyingine Waziri Lugola amesema sheria,taratibu na mila za kitanzania ,Serikali haiwezi kuruhusu wafungwa walio katika ndoa kufanya mapenzi magerezani.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post