MKE WA KISENA KUUNGANISHWA NA MUMEWE KESI YA UHUJUMU UCHUMI


Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imepanga Aprili 23 kumuunganisha, Florencia Membe mke wa Robert Kisena katika kesi ya  uhujumu uchumi inayomkabili mumewe na wenzake watatu.

Membe ambaye ni mkurugenzi wa kampuni ya Zenon Oil Gas Limited, anakabiliwa na mashtaka saba ikiwamo uhujumu uchumi na utakatishaji wa fedha zaidi ya Bilioni 2.4.

Alifikishwa mahakamani hapo wiki iliyopita, akikabiliwa na mashtaka  hayo.

Kuunganishwa kwa Kisena na mkewe kulielezwa jana na Wakili wa Serikali, Wankyo Simon mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

Wakili Wankyo alieleza kuwa shauri hilo limeitishwa kwa ajili ya kutajwa lakini washitakiwa wawili ambao ni Kulwa Kisena na Charles Seleman hawajafika wanaumwa

Pia ameeleza kuwa upelelezi shauri hilo haujakamilika, kwa sababu baadhi ya washitakiwa wanatafutwa na mmoja ambaye ni Mke wa Kisena amepatikana na watamuunganisha na mumewe.


"Upelelezi bado haujakamilika kwa sababu bado tunaendelea kutafuta washtakiwa wengine na niseme tu tumeshampata mmoja ambaye ni Florencia Membe, hivyo tunaomba tarehe ijayo aunganishwe katika kesi hii ya uhujumu uchumi namba 11/2019 inayomkabili mumewe na wenzake watatu," alieleza Simon.

Hakimu Simba alikubaliana na ombi la  upande wa mashtaka na kuahirisha kesi hiyo hadi Aprili 23 itakapotajwa.


Kisena na wenzake watatu wanakabiliwa na mashtaka 19 likiwemo la utakatishaji fedha na kuusababishia Mradi wa UDART hasara ya zaidi ya Sh.Bil 2.41

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Kulwa Kisena(33), Charles Newe(47) na raia wa China, Cheni Shi (32).


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post