MSAJILI VYAMA VYA SIASA AANZA KUICHAMBUA BARUA YA ACT- WAZALENDO


Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza, amesema wanaifanyia kazi barua ya Chama cha ACT-Wazalendo baada ya kutakiwa kujieleza kwanini kisifutwe kutokana na kukiuka taratibu na sheria na ya vyama vya siasa nchini.


Akizungumza Jijini Dar es salaam, Msajili Msaidizi Sisty Nyahoza amesema, “Tumepokea barua ya ACT ya kujibu tuliyowaandikia kwenye Machi 25, ya kuwataka kujibu hoja, ikiwamo ya kutowasilisha hesabu za ukaguzi za 2013/14, hivyo kutokidhi matakwa ya barua ya Msajili wa Vyama vya Siasa, hatua inayokiuka sheria ya vyama vya siasa sura ya 258,”.

Aliongeza kuwa kutokana na hali hiyo, barua hiyo itafanyiwa kazi kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa ili waweze kutoa haki kulingana na matakwa ya kisheria.

Machi 25, 2019 Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, alitishia kukifutia usajili Chama cha ACT-Wazalendo, kutokana na kukiuka Sheria ya Vyama vya Siasa ikiwamo kuchoma moto bendera ya Chama cha Wananchi (CUF).

Mtungi kupitia barua yake kwa ACT Wazalendo, alitoa siku 14 kwa chama hicho kuwasilisha maelezo ya maandishi kuwa ni kwanini usajili wake wa kudumu usifutwe kutokana na kukosa sifa kukiuka Sheria za Vyama vya Siasa na kutowasilisha ripoti ya ukaguzi kuanzia mwaka 2013 hadi 2017.

Taarifa iliyotolewa na Msajili wa Vyama vya Siasa Machi 25, imesema kutowasilisha ripoti ya ukaguzi ya mwaka wa fedha 2013/14, chama hicho kinakuwa bado hakijakidhi matakwa ya Msajili wa Vyama vya Siasa na hivyo chama hicho pia kinakuwa kimekiuka Sheria ya Vyama vya Siasa Sura ya 258.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post