NDUGAI ATAKA CAG AKAJIELEZE KWA RAIS....PROF. ASSAD AKAZA ' REJEA KATIBA..KUJIELEZA HAIMO"


 Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Job Ndugai jana alitumia mkutano wake na waandishi wa habari kujibu kauli ya Profesa Mussa Assad kuwa ataendelea kutumia neno “dhaifu”, akimuonya kuwa kufanya hivyo kunaweza kusababisha matatizo zaidi.

Ndugai, ambaye alisema kauli ya profesa huyo inamuweka Rais katika wakati mgumu, pia alitoa ushauri wa jinsi ya kumaliza mzozo baina yake na Bunge, kuwa ni kwenda kwa Rais na kumwambia kuwa alikosea.

Lakini ushauri wake ulipokolewa kwa maneno mafupi na CAG-mdhibiti na mkaguzi wa fedha za serikali; rejea Katiba.

Ndugai alimtaka Profesa Mussa Assad akajieleze kwa Rais John Magufuli kwani anampa wakati mgumu lakini Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu huyo wa Hesabu za Serikali (CAG) amesema Katiba ya Jamhuri ya Muungano haina kifungu kinachomtaka akajieleze.

Hatua ya Ndugai imekuja baada ya Profesa Assad kurudia tena kauli yake kuwa “dhaifu” ni neno la kawaida la kihasibu na ataendelea kulitumia. Alisema hayo wakati akiwasomea waandishi wa habari muhtasari wa ripoti ya ukaguzi wa Serikali na taasisi zake ya mwaka 2017/18 Jumatano iliyopita.

Bunge liliazimia kutoshirikiana na Profesa Assad baada ya mkaguzi huyo kusema “udhaifu wa Bunge” wakati alipoulizwa na mtangazaji wa kituo cha redio cha Umoja wa Mataifa (UN) kuhusu kutofanyiwa kazi kwa ripoti zake zinazoibua kasoro katika utendaji serikalini, ufisadi, ubadhirifu, ukiukwaji wa kanuni za fedha na manunuzi na uzembe.

Lakini jana, Spika Ndugai alikuwa na maelezo ya jinsi Bunge linavyofanya kazi kuonyesha kuwa chombo hicho si dhaifu.

“Kama hatutaki (neno dhaifu) si unaliacha? Kama unalitaka ujiite mwenyewe,” Ndugai aliwaambia waandishi wa habari.

“Tumechukua hatua kali kwa wabunge wenzetu kama Halima Mdee (Kawe-Chadema) kwani hatuwapendi? Kama utaendelea tutakuita tena na itakuwa hatari.”

Mdee amesimamishwa kuhudhuria mikutano miwili ya Bunge huku pia mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Gobdless Lema amesimamishwa mikutano mitatu wote kwa kuunga mkono kauli ya CAG.

“Zipo njia za kumaliza mambo kama haya, mojawapo aende kwa Rais akajieleze kwamba mimi nimepima nimeona nimekosea hapa na pale. Maana Rais ni sehemu yetu sisi hatuwezi kupitisha sheria bila yeye kupitisha mkono wake,” alisema.

Alisema kwa kuwa Bunge limeshapitisha azimio la kutofanya kazi naye, maana yake halina imani naye na hivyo alitakiwa ajiuzulu.

“Sasa hatumfundishi kazi, Mussa Assad anampa wakati mgumu Rais tu. Tutafanya kazi na ofisi ya wananchi,” alisema.

Ndugai alisema kwenye ukaguzi wa kila mwaka, huwa hakuna kipengele cha kulifanyia Bunge tathmini na kwa kuwa Profesa Assad amefanya hivyo alisema, “Kosa lake ni contempt of Parliament. Hawezi kulitukana Bunge kwa matusi ya rejareja”.

Alisema ni kweli kwamba neno hilo hutumiwa katika ukaguzi, lakini CAG hajawahi kukagua utendaji wa Bunge na kama alikagua, alifanya kwa sheria gani.

Alisema Bunge hujitathmini lakini si kukaguliwa utendaji wake.

Mara baada ya mkutano huo wa Spika Ndugai, Mwananchi lilizungumza na Profesa Assad ambaye alijibu kwa ujumbe wa maandishi akisema, Katiba haina kifungu cha kujieleza.

“Soma Katiba 143 ina disciplinary arrangements (mpangilio wa hatua za nidhamu), kujieleza haimo,” alisema Profesa Assad.

Ibara ya 143 (6) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano, inasema “Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu hatalazimika kufuata amri au maagizo ya mtu mwingine yeyote au idara yoyote ya Serikali, lakini maelezo hayo ya ibara hii ndogo hayataizuia Mahakama nayo kutumia madaraka yake kwa ajili ya kuchunguza kama Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu ametekeleza”.

Ibara ya 144(3) inasema “iwapo Rais anaona kwamba suala la kumuondoa kazini Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu kwa mujibu wa masharti ya ibara hii lahitaji kuchunguzwa” atateua Tume Maalum ambayo itakuwa na mwenyekiti na Wajumbe wengine wasiopungua wawili.

Sehemu hiyo inasema mwenyekiti na angalau nusu ya wajumbe wengine wa tume hiyo itabidi wawe watu ambao ni majaji au watu waliopata kuwa majaji wa Mahakama Kuu au Mahakama ya Rufani.

Awali katika maelezo yake, Ndugai alimsifu Profesa Assad kwa ujasiri wake huku akiufananisha na ujasiri wa mbwa kumtukana mtu anayemlisha.

Aliendelea kusema pia kuwa hana chuki binafsi na Assad bali tatizo ni lugha tu.

“Unatukana hadi mkono unaokulisha, inahitaji ujasiri na jamaa ana ujasiri,” alisema.

Na Elias Msuya, Mwananchi 

Tazama Video hapa

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post