MKUU WA MKOA, WILAYA ATAKAE MSWEKA MTU MAHABUSU BILA SABABU KUCHUKULIWA HATUA


Waziri wa Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, George Mkuchika amesema kuwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya wenye tabia ya kuwasweka mahabusu watu wasiokuwa na hatia watachukuliwa hatua.

Mkuchika amesema kuwa mtu nawekwa ndani kama ana hatarisha amani sio watu wanadaiana madeni huko una muweka ndani, mtu asiwekwe mpaka awe amehatarisha amani.

“Hawatatetewa na  Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Ninamshukuru mwanasheria mkuu wa Serikali ametoa waraka kwa wote waliopewa mamlaka ya kuweka mtu ndani na mimi kanipa nakala, ikieleza mazingira ya mtu kuwekwa ndani,” amesema Mkuchika leo Jumatatu Aprili 15, 2019 bungeni jijini Dodoma.

Akiwa anajibu hoja za wabunge walizozitoa katika mjadala wa bajeti hiyo mwaka 2019/2020 Mkuchika amesema, “Moja awe ametenda kosa la jinai, na (mkuu wa wilaya, mkoa) uweke kwa maandishi kwa nini umemuweka ndani. Utawala bora unasema kesi ikiwa mahakamani hakuna mkuu wa wilaya, mkoa au waziri anayeweza kuisikiliza.”

“Mahakama ya chini uamuzi wake unaweza kutenguliwa na mahakama ya juu wengine wamejiingiza katika matatizo kwa mambo ambayo tayari yametolewa hukumu mahakamani.”

Mkuchika amesema wakuu wa wilaya na mikoa wanapotumia mamlaka yao kuweka mtu mahabusu kwa saa 24 na 48 wazingatie sheria ya Tawala za Mikoa ya mwaka 1997.

“Sheria hii inawapa mamlaka kuwaweka ndani watu pale inapothibitika anahatarisha amani. Nawaomba wabunge tusikilize sheria na nawaomba na huko walipo (wakuu wa wilaya na mikoa) wanisikilize,” amesema.

“Mtu anawekwa ndani kama amehatarisha amani, si watu wanadaiana madeni hawataki kulipa unawapeleka kwa mkuu wa mkoa, hawa wanadaiana si kuhatarisha amani.”

Alisema viongozi hao wakitekeleza hatua kinyume na utaratibu wanaweza kuchukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kushtakiwa binafsi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527