ASKARI POLISI 8 KIZIMBANI KWA KUTOROSHA MADINI


Watuhumiwa 12 wakiwemo wafanyabishara wanne na Askari Polisi nane waliohusika na utoroshaji wa madini ya dhahabu kilo 319.59 yenye thamani ya shillingi bilioni 27 kinyume na sheria ya usafirishaji wa madini nchini, leo wamefikishwa tena katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Mwanza.

Kesi hiyo namba 3 ya mwaka 2019 ya uhujumu uchumi, rushwa pamoja na utakatishaji fedha inayowakabili watuhumiwa kumi na mbili wakiwemo wafanyabishara wanne na askari polisi nane, ambapo leo hii ikiwa ni mara ya 3 wamefikishwa tena katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Mwanza na kutajwa na hakimu mkazi Gwai Sumayi.

Akizungumza nje ya Mahakama wakili wa utetezi Steven Makwega anaewatetea watuhumiwa namba 1 hadi 12 ameiomba mahakama kufuata kalenda ya mahakama kutokana na kesi hiyo kutotajwa Februari 25 kama ilivyokuwa imepangwa.

Kwa upande wake Hakimu Mkazi Gwayi Sumayi, ametaka kuwepo mawasiliano baina ya wakili wa serikali na mawakili wakujitegemea wanaosimamia kesi hiyo kutokana na sintofahamu iliyotokea Februari 25 baada ya kesi hiyo kutotajwa.

Watuhumiwa wote 12 hawakutakiwa kujibu chochote kutokana na Mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa kusikiliza kesi hiyo na kurudishwa rumande hadi Machi 27 mwaka huu kesi itakapotajwa tena.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527