MBOWE : NILIPOSIKIA LOWASSA AMEHAMA NILISIKITIKA....LAKINI AKAWAAMBIE CHAMA CHAKE KISIMAMIE HAKI ZA WATANZANIA


Hatua ya Edward Lowassa, aliyekuwa mgombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) imemsikitisha Freeman Mbowe, mwenyekiti wa chama hicho Taifa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo tarehe 15 Machi 2019 Mbowe amesema, kazi ya Chadema na upinzani kwa ujumla ni kutengeneza wanachama wapya na kwamba, Lowassa alikuwa mwanachama mpya.

Hata hivyo amesema, alipopata taarifa kuwa, Lowassa ambaye pia ni Waziri Mkuu aliyejiuzulu amerejea Chama Cha Mapinduzi (CCM) alisikitika.

“Niseme ukweli kuwa, nilipopata taarifa kuwa Lowassa amehama nilisikitika,” amesema Mbowe na kuongeza kwamba “nikisema nilifurahi, nitakuwa muongo,” amesema Mbowe.

Lowassa alirejea CCM tarehe 1 Machi 2019 ambapo alipokewa na Dk. John Magufuli, Mwenyekiti wa CCM-Taifa na viongozi wengine katika ofisi ndogo ya chama hicho iliyopo Lumumba, jijini Dar es Salaam.

Mbowe amesema, kazi ya Chadema ya kupigania haki na demokrasia inahitaji kujitoa, hivyo kama kuna mtu yeyote anaona wajibu huo ni mzito ni bora asiwepo.

“Kupinga uovu kuhubiri haki na yaliyo mema na kulaani yasiyo haki, katika kuifanya kazi kunahitaji kujitoa sana sio mchezo, kazi hii sio rahisi .

“Kwa sababu lengo letu ni kusimamia haki kupitia demokrasia ni bora asiwepo kuliko kuwepo… unapoona maovu usikemee, unapoona watu wanagongwa bila sababu usikemee, unapoona watu wanapigwa risasi ukakaa kimyaa, ni bora ukishindwa kulia na sisi usiwe na sisi,” amesema Mbowe.

Mbowe amesema, wapo watu alioanza nao waliishia katikati na wale aliowakuta katikati wakashindwa hivyo haoni ajabu kwa Lowassa kuondoka.

”…Wapo tulioanzanao wakashindwa katikati, wapo tuliowakuta katikati wakashindwa pia. Hivyo mtu yeyote ambaye anaona wajibu huu ni mzito ni bora asiwepo kuliko kuwepo,”amesema Mbowe.

Mbowe ameeleza kuwa, vyama vyote vinakusanya watu kwa mahitaji maalumu na kwamba watu hao pia wanakuwa na malengo yao, ndiyo maana wanaingia na kuondoka.

”Nitoe tamko la chama kuhusu aliyekuwa mgombea wetu wa mwaka 2015, Lowassa baada ya kurudi CCM. Vyama vyote vinakusanya watu kwa mahitaji maalumu na watu hao wanakuwa na mambo yao pengine kutaka kuwatumikia watu au tamaa ya madaraka, kila mmoja ana sababu zake,” amesema Mbowe.

Aidha, Mbowe alituma ujumbe kwa Lowassa akimtaka aishauri CCM kwa kuiambia ukweli kuhusu kusimamia haki za Watanzania.

“Nilivyosikia amehama Lowassa nilisilitika niseme ukweli lakini Lowassa akawaambie ukweli chama chake kisiwatese Watanzania na wala chama hiki hakitamwaga damu. Chama cha siasa kama dodoki ukiliweka kwenye maji machafu litanyonya ukiliweka kwenye maji masafi litanyonya,” amesema.

Chanzo - Mwanahalisionline

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post