VIONGOZI WA DINI WATAKIWA KUACHA KUPOTOSHA JAMII KUHUSU UKIMWIMwezeshaji wa Huduma za VVU na UKIMWI katika jamii kutoka Manispaa ya Shinyanga, Mwita Thomas.

Viongozi wa dini wameombwa kuacha kupotosha jamii kuhusu Virusi Vya UKIMWI na UKIMWI kuwa mtu anayeishi na VVU akiombewa virusi vinapotea mwilini. 

Ombi hilo limetolewa leo na watoa Huduma za VVU na UKIMWI mkoani Shinyanga, wakiwa kwenye warsha ya kuwajengea uwezo ili kuboresha huduma katika vituo vya tiba na matunzo (CTC) iliyoandaliwa na Asasi ya kitaifa inayolenga kutokomeza UKIMWI kwa watoto na familia, Ariel Glaser Pediatric AIDS Healthcare Initiative (AGPAHI). 

Walisema baadhi ya Viongozi wa dini wamekuwa wakiwadanganya watu wanaoishi na maambukizi ya VVU waache kutumia dawa za kupunguza makali ya VVU (ARVs) kwa madai kuwa maombi yanawaponya. 

“Baadhi ya Manabii wanaibuka wanasema wamekuombea,umepona kabisa, hii ni hatari sana kwani wanachangia wateja kupotea katika huduma,hii inaumiza sana na kuua watu, naomba waache”,alisema Deo Mabula kutoka Kahama. 

“Viongozi wa dini wa namna hii wanachangia kuwepo kwa vifo, afya za wenye maambukizi ya VVU zinadhoofika ,sasa unajiuliza huyu mtu anasema kaombewa na amepona mbona hakuna uwiano wa afya yake na hicho anachosema?”,alihoji Kanzaga Fabian kutoka Msalala. 

Naye Modester Mathias kutoka Manispaa ya Shinyanga, aliwataka wananchi kuachana na imani za kishirikina kwa kudai wamerogwa na kukimbilia kwa waganga wa kienyeji matokeo yake afya zao zinadhoofika na kufa huku akiwashauri wanaoishi na maambukizi ya VVU kuendelea kutumia dawa hata kama wanaombewa na viongozi wa dini. 

Hata hivyo, Mwezeshaji wa Huduma za VVU na UKIMWI katika jamii kutoka Manispaa ya Shinyanga, Mwita Thomas, alisema kutokana na kwamba kila mtu ana imani yake, aliwashauri wanaoambiwa wamepona baada ya kuombewa, wafike wenye vituo vya afya kupima afya zao ili kuthibitisha badala ya kuacha kutumia dawa. 

“Tunashauri baada ya kuombewa na kuambiwa wamepona basi waje kwenye vituo vya afya wajiridhishe kuwa kweli wamepona kwa kupima tena VVU , vipimo ndivyo vitathibitisha kama kweli amepona, ndiyo anaweza kuacha kutumia dawa”,alisema Mwita.

“Sisi hatukatazi mtu kuombewa kwa sababu kila mtu ana imani yake, kinachothibitisha kuwa huna maambukizi ni vipimo, wewe ombewa kadri ya imani yako kisha kapime kuthibitisha kama huna maambukizi", aliongeza Mwita.
Mwezeshaji wa Huduma za VVU na UKIMWI katika jamii Manispaa ya Shinyanga, Mwita Thomas akizungumza wakati wa warsha ya Watoa Huduma za VVU na UKIMWI mkoa wa Shinyanga yenye lengo la kuwajengea uwezo ili kuboresha huduma katika vituo vya tiba na matunzo (CTC) iliyoandaliwa na Asasi ya kitaifa inayolenga kutokomeza UKIMWI kwa watoto na familia, Ariel Glaser Pediatric AIDS Health Initiative (AGPAHI). - Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Mtoa Huduma za VVU na UKIMWI , Kanzaga Fabian kutoka kituo cha afya Segese halmashauri ya wilaya ya Msalala akielezea jinsi baadhi ya viongozi wa dini wanavyochangia wateja kupotea katika huduma baada ya kuambiwa kuwa wamepona UKIMWI baada ya kuombewa.
Mtoa Huduma za VVU na UKIMWI , Deo Mabula kutoka halmashauri ya Mji Kahama akielezea jinsi baadhi ya viongozi wa dini wanavyochangia vifo vinavyotokana na UKIMWI.
Washiriki wa warsha hiyo wakiwa katika kazi ya kikundi wakijadili kuhusu mpango kazi wao katika kuhakikisha wanaboresha huduma za afya katika vituo vya tiba na matunzo. Kulia ni Consolatha Kapela kutoka halmashauri ya wilaya ya Shinyanga akichangia hoja.
Kazi ya vikundi ikiendelea.
Washiriki wakiwa katika kazi za vikundi.

Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post