NAPE NNAUYE : HAKUNA CCM IMARA KAMA HAKUNA UPINZANI IMARA

Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye akizungumza wakati wa mahojiano mubashara katika kipindi cha Clouds 360 kinachorushwa na televisheni ya Clouds, jijini Dar es Salaam jana. Kulia ni mtangazaji wa kipindi hicho, Baby Kabaye. Picha na Clouds TV 
***
Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye amesema siasa si ugomvi na kwamba “hakuna CCM imara kama hakuna upinzani imara.”

Akizungumza jana katika mahojiano maalumu katika kipindi cha Clouds 360 kinachorushwa na Clouds TV, Nape alisema siasa hazitakiwi kuwa ugomvi ila kushindana kwa hoja.

Nape, ambaye akiwa katibu wa itikidi na uenezi wa CCM kabla ya uchaguzi mkuu wa 2015 alikuwa akiponda vyama vya upinzani jana alionekana kuwa na msimamo wa kati kuhusu upinzani nchini.

Alisema “hakuna CCM imara kama hakuna upinzani imara, tunategemeana na namna ya kutegemeana ni kushindana kwa hoja.

“Kwenye siasa nadhani tusiende kwenye kugombana bali kubishana kwa hoja na inapotokea mnapishana iwe ni kwenye kuboresha si kuchukiana na mabishano hayo si mabaya wala uadui na isichukuliwe kwamba mtu anayejadili kwa misimamo hiyo asionekane anapinga.”

Akizungumzia misimamo yake, Nape alisema “nina misimamo yangu, unaweza kutafsiri utakavyoelewa ila ukweli nikiamini la kwangu nalisimamia, ukitaka niamini lako nishawishi kwa hoja naweza kuelewa na kubadilika kulingana na hoja utakazokuja nazo. Ndio hapo ninapopishana na watu wengi wakisema nina msimamo mkali, naamini mwanasiasa mzuri ni mwenye kujenga na kubomoa hoja ya mwenzako tukiishi hivyo tutakwenda vizuri,” aliongeza

Kauli ya goli la mkono

Akizungumzia kauli aliyoitoa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka 2015 kwamba CCM ingeshinda hata kwa goli la mkono, Nape alisema amekubali kwenda kaburini na msamiati wa ‘goli la mkono.’

Alisema wakati anasema hayo hakuwa na maana ambayo watu wengi wameelewa na kutafsiri hivyo.

“Nimekubali kama kuna alama ninayo mgongoni kwangu labda nitaenda nayo kaburini ni hili la goli la mkono na hata mzee (aliyekuwa katibu mkuu wa CCM- Abdurahman) Kinana aliniambia mapema kabla halijaandikwa kwamba wakati nililosema na mazingira niliyosema basi nijiandae kubeba mzigo mkubwa, nijiandae kulibeba nami nikajiandaa kisaikolojia nimelibeba hadi leo.”

“Nia yangu haikuwa mbaya ilikuwa ni kueleza kwamba kwenye ushindani inaweza kutokea mazingira wewe uliyefungwa huridhiki na kufungwa kwako lakini refa kama hajaona basi ndio umeshafungwa,” alisema.

Kuhusu bastola

Zikiwa zimepita siku 697 tangu aonyeshwe bastola mbele ya umati wa watu, mbunge huyo wa Mtama (CCM) amesema anawafahamu wote waliopanga na kutekeleza kitendo hicho lakini ameamua kusamehe.

Tukio hilo la Nape lilitokea Machi 23, 2017 nje ya Hoteli ya Protea jijini Dar es Salaam alipokwenda kuzungumza na wanahabari baada ya kutenguliwa katika nafasi ya uwaziri wa habari, utamaduni, sanaa na michezo.

Kabla hajashuka kwenye gari siku hiyo, walifika watu wakiwa kwenye gari waliovalia kiraia kisha wakamtaka Nape asishuke kabla ya mmoja wao kutoa bastola.

Nape alitenguliwa uwaziri siku chache baada ya kukabidhiwa ripoti ya kamati aliyoiunda kuchunguza tukio linalodaiwa kufanywa na mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda la kuvamia kituo cha Televisheni na Radio cha Clouds (CMG).

Alipanga kuiwasilisha ripoti hiyo kwa uongozi wa juu kwa hatua zaidi kuchukuliwa, lakini kabla hajafanya hivyo aliwekwa kando na nafasi yake kuchukuliwa na Dk Harrison Mwakyembe.

Jana, akijibu swali la mmoja wa watangazaji wa kipindi cha Clouds 360 aliyetaka kujua hatua alizochukua baada ya tukio hilo, Nape alisema anawafahamu wote waliohusika katika mpango huo lakini ameamua kuwasamehe licha ya kuwa wanasheria walishamfuata kumshawishi afungue kesi.

“Nimelelewa na mchamungu, wakati mwingine unapofanyiwa jambo linaloumiza moyo njia nzuri ni kusamehe, niliwasamehe hivyo nilimsamehe aliyenitolea bastola.”

“Nimewasamehe wote waliohusika katika utaratibu mzima, nawafahamu waliopanga na waliosimamia utekelezaji wa jambo lile, niliwasamehe wote kwa kuwa sikuona kama ingekuwa na matokeo mazuri,” alisema Nape.

Akisisitiza Napa alisema, “Nawajua si watu wa mtaani, sikuripoti polisi kwa kuwa wakati wanafanya, polisi walikuwepo, akiwemo kamanda wa polisi mkoa. Aliyetoa bastola sidhani kama alikusudia kufikia huko nadhani alipaniki na kibinadamu nikaona nimsamehe tu.”

Kuhusu uamuzi wa kufanya mkutano na wanahabari saa chache baada ya kutenguliwa uwaziri, Nape alisema alikuwa na nia njema ya kutuliza hali ya hewa

“Asilimia 99 ya watu niliozungumza nao walinishauri nisifanye ule mkutano na wanahabari lakini mwisho wa siku mwamuzi nilikuwa mimi, niliona ni wakati sahihi.”

“Nilikuwa naiona kesho lile jambo lilikuwa kubwa na linagusa media (vyombo vya habari) ambayo imekamata mioyo ya watu ndio maana nilitaka kulifunga suala hilo ili mjadala mzito usije kuibuka baadaye ambao ungeniumiza na mimi,” alisema.

“Nilitamani ule mkutano ungeenda vizuri maana ulikuwa na nia njema ya kuweka sawa mwonekano wa Serikali na chama changu (CCM), sikuwa na nia ya kumchafua mtu tena nilitaka nimshukuru Rais (John Magufuli) na niliandika kabisa nilichotaka kusema nikawaonyesha baadhi ya watu wakaona iko sawa, nimefika pale nakuta vijana wamejipanga,” alisema Nape.

Nafasi yake CCM

Alipoulizwa amejiandaa vipi endapo jina lake litakatwa kutetea kiti chake mwaka 2020, alisema haoni cha kumzuia kuwania nafasi hiyo.

“Sioni kuondolewa kwangu kushiriki uchaguzi 2020, anayeweza kunifanya nisiwe mbunge ni Mungu au mimi mwenyewe kuamua,” alisema na kuongeza

“Sioni kama chama changu kina shida, nimetekeleza ilani ya chama kwa kiasi kikubwa ila tutavuka mto tukifika wakati wake.”

Chanzo- Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post