FAMILIA YAPINGA RIPOTI YA POLISI KIFO CHA MWANAHARAKATI CAROLINE....YASISITIZA KAUAWA NA WASIOJULIKANA


Mwanaharakati Caroline Mwatha enzi za uhai wake
Baba na marafiki wa marehemu mwanaharakati Caroline Mwatha wamepinga ripoti ya polisi inayodai marehemu aliaga dunia akijaribu kutoa mimba yake

Wanasema mwenzao aliuawa kutokana na kazi yake ya kutetea haki za binadamu na kwamba jinsi mwili huo ulivyoletwa katika chumba cha kuhifadhia maiti ni suala linalotatanisha.

Caroline Mwatha mwanaharakati aliyekuwa ametoweka alipatikana akiwa maiti katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Citry mnamo Jumanne, Februari 12,2019 huku polisi wakisema kifo chake kilisababishwa na jaribio la kutoa mimba.

Mama huyo wa watoto wawili alitoweka na kisa hicho kuripotiwa katika Kituo cha Polisi cha Buruburu mnamo Jumatano, Februari 6, baada ya kumpeleka mwanawe shuleni.

 Kulingana na marafiki wa Mwatha, polisi wanafahamu ni nini kilimtokea marehemu kwa kuwa alichukuliwa na watu wasiojulikana kutoka nyumbani kwake.

 Akizungumza na wanahabari nje ya chumba cha maiti cha City, baba ya marehemu, Stanlus Mbai, alidai bintiye aliuawa kwa sababu ya kazi yake ya kutetea haki na ufichuzi kuhusu ufisadi eneo la Dandora, Kaunti ya Nairobi.

 "Hakika mbele zake Mungu, Caroline aliuawa kwa sababu ya kuamini katika ukweli, kifo chake hakijasababishwa na ugonjwa wala ajali, aliuawa kwa sababu ya kazi yake," baba yake Mwatha alisema.

 Bw Mbai alisema kwamba, mwanawe alihofia maisha yake na hivyo hakutaka wazazi wake kumfahamisha yeyote kuhusu kazi yake.

 Baba yake marehemu alihoji jinsi mwili wa marehemu ulivyowasilishwa katika chumba cha maiti cha City na ni mwanamume yupi huyo anayedaiwa kumpeleka Hospitali Kuu ya Kenyatta.

"Badala ya kuandika Caroline Mwatha, jina lake liliandikwa Caroline Mbeki, aliletwa City na mwanamke, twafahamu mwanzo alipelekwa Hospitali Kuu ya Kenyatta na mtu anayedai ni mume wake, mume wa Caro alikuwa Dubai wakati huo," baba alisema.

 Wakati huohuo, baba ya marehemu alidai kupokea simu kutoka kwa mtu asiyejulikana akimuuliza wapi alipofikia na shughuli ya kumsaka mwanawe, baadaye mwili ulipatikana City.

 Kilio cha baba kiliwahuzunisha hata na marafiki zake marehemu waliounga mkono kauli zake na kudai polisi wanafahamu kilichomtokea mwenzao.

 Inadaiwa kwamba, marehemu alichukuliwa nyumbani kwake kwa sababu ya kazi yake.

 "Caro ameaga kwa sababu ya kupigania haki za vijana, na polisi wanafahamu alivyokufa. Tunawataka watetezi wa haki za binadamu wote kutohofu kwa sababu kilichomtokea Caroline Mwatha kinaweza mtokea yeyote kati yetu" mmoja wa marafiki alisema.

Aidha kuna madai kutoka kwa marafiki zake marehemu kuwa, sajili waliyoikuta awali sio waliyoikuta wakati wa kuusaka mwili wa marehemu. 

Mama huyo wa watoto wawili alitoweka na kisa hicho kuripotiwa katika Kituo cha Polisi cha Buruburu mnamo Jumatano, Februari 6, baada ya kumpeleka mwanawe shuleni. 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post