MAWAZIRI 8 WAJITOSA MGOGORO WA ARDHI KATI YA JWTZ NA WANANCHI JIJINI MWANZA

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, ambaye ni mwenyekiti wa kamati maalumu ya kushughulikia migogoro ya ardhi, amewataka wakazi wa Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza wenye migogoro ya ardhi na taasisi za jeshi na uwanja wa ndege kuwa watulivu, baada ya Rais John Magufuli  kuagiza umalizwe.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Shibula wilayani humo, Lukuvi alisema Rais ameunda kamati hiyo kwa ajili ya kusikiliza mgogoro wa mitaa 11 na kupata ufumbuzi ambao utawezesha wananchi kulipwa fidia.

"Hapa Mwanza mgogoro ni mkubwa sana baina ya Uwanja wa Ndege, Jeshi la Wananchi (JWTZ) na wananchi ambao unahusisha mitaa 11, ndio maana sisi tumekuja hapa kuangalia maeneo yote ili kupata taarifa sahihi za taasisi hizo na wananchi ili tupeleka kwa Rais na kumshauri kutangaza kuwa wafuatao wataishi katika maeneo hayo milele,” alisema Lukuvi.

Aidha, aliwataka wananchi wa maeneo husika walioambiwa wasiendeleze wabaki hivyo hivyo wasijenge, ingawa serikali imesitisha shughuli za kuwaondoa.

"Tumepata taarifa nzuri kutoka kwa pande zote mbili na nyaraka za taasisi na wananchi tumezipata, hivyo tutaenda kukaa na kutoa maamuzi yaliyo na tija kwa jamii, maeneo mengi tumepita migogoro mingi ni ya vijiji na hifadhi, lakini hili la Mwanza limekuwa tofauti,” alisema Lukuvi.

Lukuvi alisema migogoro ya ardhi haitaisha katika wilaya za Ilemela na Nyamagana kutokana na kushindwa kupima ardhi, hali iliyosababisha wananchi kuvamia maeneo kutokana na uzembe wa halmashauri hizo.

Akisoma taarifa ya mitaa mitano ya Kata ya Shibula, Katibu wa Kamati ya kushughulikia migogoro Robert Luzili, alisema uwanja huo wa ndege ulihamishwa kutoka Sabasaba mwaka 1952 hadi 1958, ukajengwa eneo la Kisaka Kata ya Ilemela na wananchi kufidiwa kwa kulipwa na serikali katika vitongoji vya Kisaka, Bukungu na Buduku.

"Sisi hatuna pingamizi lolote juu ya kuhamishwa endapo serikali itatulipa fidia na kutuonyesha maeneo halali ya kujenga, maana mpaka sasa tunamaisha ya shida, tumeshindwa hata kuendele kimaisha nyumba taturuhusiwi kujenga wala kulima tunamwomba Rais atatulie tatizo hilo,” alisema Luzili.

Katika ziara hiyo ya mawaziri nane ambao walifuatana na Lukuvi ni Luhaga Mpina (Mifugo na Uvuvi); Hussen Mwinyi (Ulinzi na JKT); Prof. Makame Mbarawa (Maji na Umwagiliaji); Hamisi Kigwangalla (Maliasili na Utalii); Selemani Jafo (Tamisemi); manaibu mawaziri Omary Mugumba (Kilimo) na Mussa Sima (Mazingira).

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post