MAHAKAMA YATENGUA NGOME YA LIPUMBA NA MAALIM SEIF


Mahakama Kuu nchini Tanzania, leo imetoa uamuzi wa kesi kuhusu mvutano wa wajumbe wa Bodi ya Wadhamini ya Chama Cha Wananchi (CUF), ikiwakataa wajumbe wapya waliokuwa wameteuliwa na timu Lipumba [Profesa Ibrahim] na timu Seif [Maalim Sharif Hamad].

Kupitia hukumu yake iliyosomwa leo jijini Dar es Salaam, Mahakama Kuu imeeleza kuwa wajumbe wa pande zote mbili hawakukidhi vigezo vya kuwa wajumbe wa Bodi ya Wadhamini, hivyo uteuzi wao umetenguliwa.

Aidha, ingawa wajumbe wa pande zote mbili wamekataliwa, uamuzi huo umepokelewa kama ushindi na kambi ya Maalim Seif, kwani ina maanisha kuwa wajumbe waliokuwepo awali wanaendelea licha ya muda wao kuisha, hadi pale uchaguzi mwingine utakapofanyika.

Katika kesi ya Msingi, Mbunge wa Malindi (CUF), Ally Saleh alikuwa akipinga uamuzi wa Wakala wa Usajili, Udhamini na Ufilisi (RITA) kuwapitisha wajumbe waliopendekezwa na kambi ya Profesa Ibrahim Liumba kuwa wajumbe wapya wa bodi hiyo.

Profesa Lipumba ndiye mwenyekiti wa CUF anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa. Mgogoro wa madaraka ndani ya chama hicho uliibuka baada ya Profesa Lipumba kutangaza kuahirisha uamuzi wake wa kujiuzulu nafasi ya Uenyekiti katika harakati za kampeni ya uchaguzi Mkuu, mwaka 2015.

Chama hicho hivi sasa kimegawanyika katika kambi hizo mbili, hali inayoathiri utendaji pamoja na kuzuka kwa mgogoro wa matumizi ruzuku.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post