SERIKALI YATOA SABABU ZA KONDOMU KUADIMIKA MITAANI

Baada ya kuwapo kwa malalamiko ya upungufu wa kondomu katika baadhi ya maeneo nchini, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile, amesema wana taarifa juu ya suala hilo na kwamba hatua za haraka zimeanza kuchukuliwa.

“Changamoto imetokea, baada ya kubadilisha mfumo uliokuwapo kwa wale wasambazaji wa taasisi binafsi, jukumu hilo limerudi ndani ya wizara, hivyo kuanzia sasa ndiyo itakuwa inasimamia manunuzi, usambazaji wa mipira ya kiume.

“Utaratibu uliokuwapo (awali) kulikuwa na baadhi ya taasisi ambazo zilikuwa zinapewa fedha na kununua mipira kisha kuisambaza kwa bei nafuu, ndiyo maana zilikuwa zinapewa majina mbalimbali kupitia hizo taasisi.

“Utaratibu wetu Serikali tutakuwa tunanunua mipira hiyo na kuigawa kwenye vituo mbalimbali vya kutolea huduma za afya na kwenye jamii

“Hivyo tumelibaini hilo tatizo katika kipindi hiki cha mpito, kwa kushirikiana na wenzetu tutahakikisha tuna kondomu za kutosha ndani ya wiki moja, kuanzia sasa zitakuwa zimeanza kupatikana,” alisema.

Alisema si kweli kwamba zimepanda bei na Serikali itaendelea na utaratibu kuhakikisha zinapatikana za kutosha na kuzisambaza ili watu waendelee kujikinga.

“Taarifa hii kwetu ni nzuri, inaonesha matumizi yapo na mahitaji yapo, tumebaini na tunashughulikia hili,” alisema Dk. Ndugulile.

Baadhi ya maeneo yanayodaiwa kuwa na upungufu huo ni mji wa Njombe.

Njombe ndiyo mkoa wenye kiwango cha juu cha maambukizi ya VVU kwa asilimia 11.4 ukifuatiwa na Iringa wenye asilimia 11.3 kulingana na takwimu za Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids).

Credit: Mtanzania

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post