BALOZI AMPIGA MAKOFI ASKARI WA USALAMA BARABARANI

Wanaharakati na spika wa bunge la Uganda wameshutumu vikali kitendo cha balozi wa Uganda nchini Burundi, Meja Jenerali Matia Kyaligonza kumpiga kofi askari mwanamke wa usalama barabarani mwishoni mwa wiki.

Picha za kufanyiwa fujo askari huyo zilionekana kwenye mitandao ya kijamii ambazo zimeibua hasira miongoni mwa wananchi, huku taasisi za jeshi na polisi zikimkosoa Jenerali huyo.

Mvutano kati ya walinzi wa balozi huyo na askari aliyetambulika kwa jina la Esther Namaganda aliyewazuia kukiuka sheria za barabarani ulishuhudiwa na wananchi mtaa wa Seeta.

Esther alionekana kwenye video iliyochukuliwa mtu aliyeshuhudia tukio hilo akifanyiwa fujo na balozi huyo.

Katika video hiyo iliyotumwa kwenye mitandao ya kijamii, mmoja wa askari anaonekana akiuvuta mkono wa Sajenti Esther ambaye anajaribu kukabiliana naye.

Balozi Kyaligonza, ambaye alionekana akiwa amevalia shati jeupe, alikuwa akizunguka eneo la tukio hilo akiwa ameshikilia bakora.

Msemaji wa Jeshi la Uganda, Brigadia Jenerali, Richard Karemeire ameomba radhi kwa shambulio dhidi ya Sajenti Esther.

''Tunaomba msamaha kwa askari polisi… hata hivyo habari njema ni kwamba sisi kama jeshi la Uganda tumechukua hatua za haraka kwa hao askari wawili wamekamatwa na upelelezi unaendelea kwa pamoja na polisi na baada ya hapo hatua kali zitachuliwa dhidi yao,'' amesema.

Spika na wanaharakati

Spika wa bunge la Uganda, Rebecca Kadaga amelaani vikali kitendo hicho wakati alipokutana na wanaharakati wa haki za wanawake waliowasilisha malalamiko kwake.

''Tabia hii ya kumshambulia mtu ambaye anafanya kazi aliyopewa na serikali haikubaliki miongoni mwa viongozi na mtu mwingine yeyote haikubaliki, nafurahi kwamba wahusika wamekamatwa na ningemtaka mkuu wa jeshi la polisi kumpandisha cheo mwanamke huyo,''

Angela Asiimwe msemaji wa kundi la wanaharakati wa haki za wanawake nchini Uganda alisema ''Ulikua ni ukiukaji mkubwa wa haki zetu wanawake na Waganda kwa ujumla, nafurahi kwamba baadhi ya waliompiga Sajenti Namaganda wamekamatwa.''

Chanzo - Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post