MKURUGENZI ITIGI NA WENZAKE 6 KUENDELEA KUSOTA RUMANDE


Mkurugenzi Mtendaji (DED) halmashauri ya mji wa Itigi, wilayani Manyoni mkoani Singida, Pius Luhende na wenzake sita wanaokabiliwa na kesi ya mauaji ya mkulima Isaac Petro (28) wataendelea kukaa rumande hadi Machi 11, mwaka huu kesi yao itakapotajwa tena.

Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Askari Wanyamapori wa halmashauri Rodney Elias (42), Askari wa Wanyamapori Hifadhi ya Doloto wilayani Manyoni, Makoye Steven, Mwanasheria wa halmashauri hiyo, Eric Paul (31) na Ofisa Tarafa Itigi, Eliutha Augustino (43).

Wengine ni Ofisa Kilimo na Mifugo, Silvanus Lungwisha (50) na Ofisa Mtendaji wa kijiji cha Kazikazi, Yusuph John (25).

Wakili anayemtetea mshitakiwa Luhende, Victoria Revocati ameuomba upande wa mashitaka kuharakisha upelelezi ili mteja wake aweze kupata haki yake mapema kutokana na ukweli kuwa kesi hiyo haina dhamana.

Hata hivyo, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Consolata Singano alimweleza mshitakiwa huyo kupitia kwa Wakili wake kuwa kwa sasa bado ni mapema mno kulalamikia ukamilikaji wa upelelezi kutokana na uzito wa kesi, ambayo ni kesi ya mauaji.

Washitakiwa wote kwa pamoja wanadaiwa kuwa mnamo Februari 2, mwaka huu huko kwenye Genge namba 48 kijiji cha Kazikazi, kata ya Kitaraka tarafa ya Itigi wilayani Manyoni, walishirikiana kumuua kwa risasi mkulima wa kijiji hicho, Isaack Petro (28) kinyume na Kifungu cha 116 na 197 vya Sheria ya Kanuni za Adhabu.

Walipofikishwa Mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Februari 11 mwaka huu, Washitakiwa hawakutakiwa kujibu lolote kwa kuwa Mahakama hiyo haina Mamlaka kisheria kusikiliza shauri hilo.

Washitakiwa wote saba wamerejeshwa rumande hadi Machi 11, mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527