KULALA GUEST NJOMBE SASA LAZIMA UWE NA KITAMBULISHO


Mkuu wa wilaya ya Njombe, Ruth Msafiri amesema watu wote wanaoingia kwenye nyumba za kulala wageni ni lazima waonyeshe kitambulisho kinachotambulika na Serikali.

Msafiri ametoa kauli hiyo leo Jumamosi wakati akizungumza na maofisa ustawi wa jamii ngazi ya wilaya na kata katika semina ya Kamati ya Ulinzi wa Mwanamke na Watoto iliyokuwa ikitolewa na maofisa kutoka wizara ya afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto.

Semina hiyo pia ilitoa mafunzo ya  namna ya kukabiliana na matukio ya utekaji na mauaji ya watoto yanayoendelea wilayani Njombe.

“Katika kipindi hiki tuhakikishe tunajisimamia maeneo yetu tunayoishi. Mgeni yeyote iwe ni kijijini au mjini tutoe taarifa kwa viongozi wetu na kwenye nyumba za kulala wageni tumeshatoa maelekezo.”

“Kila anayeingia nyumba ya kulala Njombe hii awe na kitambulisho ninaamini hakuna mtu atasema hana kitambulisho cha mpiga kura au cha taifa kama huna basi wewe si raia wa Tanzania,” amesema Msafiri.

Amesema mtu ambaye hatakuwa na kitambulisho chochote kile awe na barua ya utambulisho alikotoka vinginevyo hatakubaliwa kupokelewa popote ndani ya wilaya yake.

“Tunafanya hivyo si kutaka kuwanyanyasa hapana bali ni kuona suala la ulinzi na usalama linazingatiwa na tunakuwa salama zaidi,” ameongeza.

Na Godfrey Kahango, Mwananchi 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527