Mwenyekiti wa Kamati ya Mpira wa Wanawake, Amina Karuma akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani ) wakati wa kutangaza mchuano wa ligi kuu ya soka la wanawake ya SERENGETI LITE kati ya Klabu za Simba Queens na Yanga Princess ambazo zinatarajia kukutana kwenye mchezo utakaochezwa Jumapili, Januari 13,2019.Kushoto kwake ni Afisa masoko wa kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) Bw. George Mango na kulia kwake ni Kocha wa Yanga Princess Hamis Kinonda.
Afisa masoko wa kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa kutangaza mchuano wa ligi kuu ya soka la wanawake ya SERENGETI LITE kati ya Klabu za Simba Queens na Yanga Princess ambazo zinatarajia kukutana kwenye mchezo utakaochezwa Jumapili, Januari 13,2019.Kulia kwake Mwenyekiti wa Kamati ya Mpira wa Wanawake, Amina Karuma na kushoto kwake ni Kocha wa Simba Queens Omari Mbweze.
Nahodha wa Simba Queens Mwanahamis Omar akiongea na waandishi wa habari jinsi walivyojiandaa na Mchezo huo wa watani wa jadi hapa nchini Klabu za Simba na Yanga zinatarajia kukutana kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Wanawake ya Serengeti Lite utakaochezwa Jumapili, Januari 13,2019
Kwa mara ya kwanza katika historia ya soka la Wanawake hapa nchini Klabu za Simba na Yanga zinatarajia kukutana kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Wanawake ya Serengeti Lite utakaochezwa Jumapili, Januari 13,2019.
Mchezo huo utachezwa saa 10 Jioni katika Uwanja wa Karume, Ilala makao makuu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). Ligi kuu ya wanawake inadhaminiwa na kinywaji cha Serengeti Premium Lite kwa msimu wa pili mfululizo.
Katika mchezo huo unaotarajiwa kuwa na msisimko mkubwa, kiingilio kitakuwa shilingi 2,000. Mashabiki wanahakikishiwa usalama huku vyombo husika vikihakikisha mchezo salama bila bughudha ya aina yoyote.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mpira wa Wanawake, Amina Karuma, akizungumza kuelekea mchezo huo amesema msimu huu umeanza kwa msisimko mkubwa na ushindani wa aina yake hivyo ni matarajio yake kuwa mchezo huo wa watani wa jadi utaakisi ubora wa Ligi Kuu ya Wanawake ya Serengeti Lite.
“Mchezo huo unaingia kwenye rekodi za Ligi Kuu ya Wanawake ya Serengeti Lite kwa kuwa ndio mchezo wa kwanza kuzikutanisha timu hizo tokea kuanza kwa soka la Wanawake hapa nchini,” alisema Amina.
Aidha amewataka mashabiki kujitokeza kwa wingi kushuhudia mchezo huo na kujiona vipaji pamoja na ushindani wa hali ya juu kutoka pande zote za mchezo.
Naye Afisa masoko wa Serengeti Breweries Bw. George Mango amewahakikishia wadau wa soka la wanawake, mashabiki wa mpira wa miguu kuwa kinywaji cha Serengeti Lite kimejidhatiti kuhakikisha wanapata burudani ya hali ya juu kupitia mchezo huo kama ilivyokuwa kwa michezo mingine iliyotangulia.
“Mashabiki wakae tayari kuona namna kinyaji cha Serengeti Lite kilivyo tayari kuwaletea burudani ya hali ya juu kwenye mechi hii ya kusisimua,” amesema Mango.
Serengeti Premium Lite ni bidhaa ya kwanza Tanzania kujitokeza kudhamini ligi ya wanawake, na imejidhatiti kusaidia kupandisha viwango vya ligi hii kupitia kupitia udhamani, matangazo kwenye magazeti pamoja na viwanjani.
Bia ya Serengeti Premium Lite inadhamini Ligi Kuu ya Wanawake kwa kitita cha Shilingi 450 milioni kwa kipindi cha miaka mitatu.