MBOWE,MATIKO WAITWA MAHAKAMA YA RUFAA


Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema na Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko wakiwa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam

KESI ya kupinga kurejeshewa dhamana iliyofunguliwa na serikali dhidi ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasim na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe na Mwekahazina wa Baraza la Wanawake la chama hicho (BAWACHA), Esther Matiko, itasikilizwa Mahakama ya Rufaa jijini Dar es Salaam, tarehe 18 Februari mwaka huu. 

Serikali iliwasilisha Mahakama ya Rufaa, maombi ya kuwazuia Mbowe na Matiko kurejeshewa dhamana zao. Ni baada ya Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, kutupilia mbali mapingamizi ya serikali yaliyotaka mahakama hiyo kutosikiliza shauri lililofunguliwa na Mbowe na Matiko.

Kwa mujibu wa vyanzo via taarifa kutoka Mahakama ya Rufaa na ambazo zimethibitishwa na Prof. Abdallah Safari, ambaye anaongoza jopo la mawakili katika kesi hiyo, ni kwamba “Mbowe na Matiko, watafika mbele ya majaji wa mahakama ya rufaa, Jumatatu ya tarehe 18 Februari.”

Mbowe ambaye pia ni mbunge wa Hai, mkoani Kilimanjaro na Kiongozi wa Kambi rasmi ya upinzani bungeni, alifutiwa dhamana na mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa madai ya kukiuka masharti ya dhamana aliyopewa.

Katika uamuzi wake, mahakama ilisema, maelezo yaliyotolewa na Mbowe, mdhamini wake na wakili wake, yalilenga kuidanganya mahakama.

Naye Matiko ambaye pia ni mbunge wa Tarime Mjini, alifutiwa dhamana na mahakama baada ya kushindwa kufika mahakamani kwa mara mobile mfululizo kwa maelezo kuwa alikuwa nje ya nchi kwa shughuli za Bunge.

Chanzo- Mwanahalisionline

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527