AMUACHA MUMEWE KITANDANI KISHA KUTOKA NJE NA KUJIUA KWA MTANDIO



Mkazi wa mtaa wa Nakayaya wilayani Tunduru mkoani Ruvuma, Awetu Makunula (44) amejinyonga hadi kufa kwa kutumia mtandio jirani na nyumbani kwa wazazi wake.

Mume wa marehemu Awetu, Salum Namtikwe, amesema usiku walilala wote na kabla ya tukio hilo mkewe aliamka saa 11 alfajiri na kumuaga kuwa anatoka nje kwa ajili ya kufagia nje ya nyumba yao.

Amesema baada ya kupewa maelezo hayo yeye aliendelea kulala lakini baadaye alishangaa kupata taarifa za mkewe kukutwa akiwa amejinyonga hadi kufa kwa kujining’iniza katika mti uliopo jirani na nyumbani kwa wazazi wake.

“Baada ya kupatiwa taarifa hizo niliamka na kwenda eneo la tukio na kumtambua marehemu mke wangu, baadaye tulitoa taarifa kwa viongozi wa serikali kwa ajili ya taratibu za kuuondoa mwili huo katika eneo hilo,” amesema mume wa marehemu.

Akisimulia maisha ya mkewe, Namtikwe amefunguka kuwa hajawahi kugombana naye lakini alikuwa mgonjwa wa homa za mara kwa mara licha ya kwamba siku aliyojinyonga hakulalamika kuumwa.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, ASCP Gemin Mushy amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema polisi inaendelea na uchunguzi ili kubaini chanzo cha kifo chake.

Chanzo- Eatv

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527