Dereva wa lori la mafuta mali ya Kampuni ya Lake Oil, Christopher Kikwete (42) mkazi wa Kibamba Jijini Dar es Salaam anashikiliwa na polisi mkoani Songwe kwa tuhuma za kusafirisha wahamiaji haramu 10 raia wa Ethiopia kinyume cha sheria.
Kamanda wa Polisi mkoani huo, Mathias Nyange amesema hayo jana Jumatano Januari 02, 2019 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.
Amesema dereva huyo alikamatwa Desemba 31, 2018 katika stendi ya mabasi ya Makaburini mjini Vwawa wilayani Mbozi saa 4 asubuhi wakati polisi kwa kushirikiana na Idara ya Uhamiaji wakiwa katika doria walilisimamisha lori hilo na kukuta limejaza wahamiaji hao katika kitanda kilichopo nyuma ya kiti cha dereva.
Kamanda huyo amesema lori hilo lenye namba T 500 DFJ na tera lenye namba T 833 CMN aina ya Scania ni tanki lililokuwa limebeba mafuta ya petroli kutoka Dar es Salaam kwenda nchini Zambia nalo linashikiliwa na jeshi hilo.