SERIKALI YAFUTA KODI YA PANGO LA ARDHI KWA TAASISI NA MADHEHEBU YA DINI

SERIKALI Imefuta kodi ya pango la ardhi kwa Taasisi na Madhehebu ya dini nchini kuanzia mwaka wa fedha wa 2018/2019.

Hatua hiyo imetangazwa jana Jumapili Januari 27, 2019 na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi jijini Mbeya wakati wa ibada ya kuwaweka wakfu viongozi wa Jumuiya Kuu ya Kanisa la Kibaptisti Tanzania (BCT).

Lukuvi alisema Rais Magufuli ameiagiza wizara hiyo kutoyatoza kodi madhehebu ya dini kwa sehemu ambazo zimeandaliwa kwa ajili ya kufanyia ibada.


"Rais ameagiza kuanzia Julai mosi mwaka huu wa fedha madhehebu ya dini yasilipe kodi ya ardhi kwa maeneo ambayo huduma za maombi na ibada zinatolewa, hata hivyo msamaha huu hauhusu maeneo ambayo kuna miradi ya kuingiza fedha ambayo tunajua madhehebu mengi yameanzisha," alisema Lukuvi.


Lukuvi alifafanua maagizo hayo tayari yametolewa kwa makamishna wa ardhi wa kanda na mikoa pamoja na maofisa ardhi wa majiji, manispaa na halmashauri nchi nzima.


Hata hivyo, Lukuvi ametoa nafasi ya kukutana na viongozi wa dini ambao wana migogoro ya ardhi kwenye maeneo ambayo wanatoa huduma.


"Najua kuna migogoro mingi kwenye maeneo ambayo mnatoa huduma hivyo nawakaribisha ofisini kwangu Dodoma na kama migogoro itakuwa mikubwa nitafika mpaka eneo la mgogoro," alisema Lukuvi.


“Wizara yangu imepewa jukumu la kutatua migogoro ya ardhi kabla ya mwaka 2020 na tusipotatua migogoro ya dini inaweza kupelekea uvunjifu wa amani nchini hivyo hatutaki kuifuga migogoro iliyopo,” alisema.


Awali, askofu wa kanisa la Baptisti nchini, Arnold Manase amesema kanisa lake ni moja ya madhehebu yanayoongoza kuwa na migogoro ya ardhi na baadhi ya waumini wa kanisa hilo.


"Kwa kuwa waziri mwenye dhamana upo naomba nafasi nije ofisini kwako nikueleze migogoro iliyopo ndani ya kanisa langu ili uangalie namna ya kuitatua maana migogoro imekithiri mpaka kufikia hatua ya kujenga makundi miongoni mwa waumini," alisema Manase.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527