ZITTO KABWE KUJISALIMISHA TAKUKURU KESHO

Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, kesho anatarajia kuitikia wito wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kuhusiana na mambo aliyoandika kwenye mitandao ya kijamii.

Takukuru kupitia Naibu Mkurugenzi Mkuu wake, Brigedia Jenerali John Mbungo, ilimtaka kiongozi huyo kufika ofisini kwake kutoa ushahidi wa tuhuma alizozitoa kuwa kuna kampuni tatu za chuma zimewahonga baadhi ya viongozi wa serikali.

Sehemu ya taarifa ya wito huo ilieleza kuwa: “Tunatoa taarifa hii kupitia vyombo vya habari kumwomba Zitto Kabwe afike ofisi za Takukuru Dar es Salaam mapema iwezekanavyo ili tushirikiane katika kulishughulikia suala hili muhimu kwa mustakabali wa maendeleo ya taifa letu.”

Alipotafutwa Afisa Habari wa ACT-Wazalendo, Abdallah Khamis, kueleza ni lini kiongozi huyo atakwenda kuripoti Takukuru, alisema Zitto ataripoti Takukuru Ijumaa (kesho).

Kwenye mitandao ya kijamii Zitto alidaiwa kuandika kuwa amepata habari za kushtusha kuwa kampuni tatu za China, Russia na Uturuki zimewahonga baadhi ya watendaji wa serikali kuchelewesha mradi wa Mchuchuma na Liganga. Lengo ni kuhakikisha nchi hizo zinapata soko la chuma chao.

Aliendelea kuandika kuwa kuhujumu mradi wa Mchuchuma na Liganga ni uhaini. Baadhi hawawezi kusahau hujuma hiyo na yeyote anayeshiriki atasakwa mpaka kaburini kwake, ikibidi kuondoa kinga za watu ili liwe fundisho kwa uhujumu huu uchumi na uhai wa taifa letu.

Aliandika zaidi kuwa msamaha wa kodi kwa bomba la mafuta kutoka Uganda ni mkubwa na hauna faida kulinganisha na mradi wa Mchuchuma na Liganga utakaotoa ajira za kudumu 35,000 kuingiza fedha za kigeni bilioni 4.6 kwa mwaka na kuifanya nchi yetu kuwa na viwanda vikubwa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post