JINSI WANAWAKE WENYE SHEPU WANAVYOHANGAISHA WANAUME MITAANI


Habari dada, kwa jina naitwa Warda nina miaka 26. Nina mume wangu wa ndoa tangu mwaka jana 2017. Tulishaishi mwaka mmoja bila ndoa ambayo ni mwaka 2016. 

Naomba ushauri wako, mume wangu anapenda sana wanawake wanene wenye mishepu. Mimi siyo mnene wala mwembamba ni wa kawaida tu na mume wangu nampenda sana na yeye pia ananipenda.

Lakini tatizo kubwa ni kuchepuka kila nikikaa naye namuuliza kinachomfanya achepuke ni nini ananijibu ni mahaba. Lakini mimi kila kitu namfanyia anachotaka lakini bado anachepuka. 

Ana umri wa miaka 27. Je, umri wake labda ndio unamfanya hivyo au ni nini. Maana nimechoka kumvumilia, je, nifanyeje?

Mpenzi msomaji, bila shaka umemsikia dada huyu anavyolalamika juu ya nyendo za mumewe. Kwamba mumewe anavutwa zaidi na mishepu ya wanawake kila wapitapo au awaonapo popote. 

Hili ni tatizo kubwa. Bibie amefikia hatua akaona bora apaze sauti kwa sababu anahisi kabisa kwamba mume wake havutiki tena naye bali mawazo au mapenzi kayahamishia huko mitaani anakowakodolea macho wanawake wenye mishepu.

Bibie kajieleza vema hapo juu, kwamba yeye siyo mnene ni umbo la kawaida tu. Hata hivyo, mwanaume huyo alimpenda jinsi alivyo, lakini sasa anashangaa mumewe kaipata wapi tabia ya kupenda wanawake wanene wenye mishepu na makalio mvuto.

Mpenzi msomaji, mimi nimetafakari kilio cha bibie nikaona picha iliyosheheni matukio kibao. Labda hapa nitaje machache, mengine msomaji wangu utamalizia.

Katika maisha ya ndoa, zipo changamoto mbalimbali. Pia zipo siri nyingi zilizojificha ambazo hujitokeza baadaye baada ya watu kuoana. Ni katika maeneo machache sana wawili huweka wazi tabia zao kabla ya kuoana. Mengine hufichwa yakajitokeza baadaye.

Inawezekana kabisa, tabia hii ya kupenda wanawake wenye mishepu kijana huyu alikuwa nayo lakini akalazimika kumuoa huyo anayelalamika kutokana na sababu mbalimbali. Labda alimpa mimba kabla, au ilikuwa ni shinikisha la wazazi na kadhalika.

Au, inawezekana kabisa kijana huyu hakuwa na hiyo tabia hapo awali, ila baada ya kuoa na kuchanganyika na vijana wenzake, akajikuta anaiga tabia ambazo wala hakuwahi kufikiria kuwa nazo. Akaona wenzake wanafurahia wanawake wenye mishepu na yeye akavutwa kupenda. 

Kingine inawezekana baadhi ya marafiki zake wameoa wanawake wenye mishepu na hivyo kumjaza sifa walizonazo wanawake wa aina hiyo, matokeo yake anamuona hata yule wa nyumbani aliyemchagua mwenyewe, kumbe hafai. Hiyo ni laana ya kuiga vya wengine ambavyo kwako ni madhara.

Angalia sasa kijana ambaye alikuwa anaishi vizuri na mkewe kaanza kubadilika na hata wanapokuwa matembezini pamoja bwana akiona mwanamke mwenye shepu hata kama yuko na mumewe, atageuza shingo kumtizama.

Jambo hilo limemkwaza sana bibie hata kuamua kulitoa moyoni aweze kupewa ushauri. Amefikia hatua kumuuliza mumewe kwamba kwanini anatamani vya nje wakati yeye yupo. Na akamuuliza ni nini anachokikosa kwake hata kuamua kukodolea macho vya nje?

Mpenzi msomaji, nimedokeza awali hapo juu kwamba ziko siri zilizojificha. Inawezekana kabisa mume huyu baada ya kuoa amekuja kugundua kuwa yapo mapungufu fulani kwa mkewe.

Lakini hata kama yapo mapungufu, wangeweza kabisa kuyarekebisha, maisha yakasonga mbele. 

Kingine kinachoweza kuwa moja ya sababu ya jamaa kuvutiwa na shepu ya nje, inawezekana anatoka nje ya ndoa. Na pengine kwa utashi wake mwenyewe au kwa kushawishiwa na marafiki zake, amepata mchepuko mwenye mishepu kiasi cha kumchanganya.

Ndio maana baada ya kuulizwa na mkewe kwanini anahangaika na wanawake wa nje akamjibu kuwa ni mahaba. Hapa tayari ndoa iliyokuwa na matumaini imeshaingia dosari.

Wanatiana moyo kwamba wanapendana lakini katika uhalisia ule upendo wa mwanzo umeshagawanyika na kinachotawala sasa ni mashaka na hofu hasa kwa bibie ambaye anashangaa nini kimemsibu mumewe.

Mwanaume yeye ameshaweka wazi tabia yake kwamba anapenda michepuko. Na mwanamke anadai anajitahidi kumzuia mume wake asivutwe na tamaa za nje lakini anashindwa ndio maana ameamua kuvunja ukimya.

Kiukweli, na hii nimeisema mara nyingi kwamba, shetani yuko kazini akiharibu na kubomoa ndoa za watu. Jamaa kavamiwa na pepo linalotamani wanawake wa nje ingawa wa kwake mzuri yuko ndani. 

Ili ujue shetani kamnasa mwanaume huyo, ngoja mkewe aamue kufungasha virago ndipo atakapozinduka na kujiona mjinga kwa kutamani mishepu ya mitaani isiyo na faida, iliyojaa hasara. Maisha Ndivyo Yalivyo.

Tabia za aina hii ni hatari kwani mwanamke naye aweza kuchepuka. Na huo ukawa mwanzo wa kukaribisha maradhi mabaya yanayoua na kuchipua watoto yatima. 

Je, una ushauri wowote kwa familia hii? Au unalo suala la kifamilia/ndoa/mahusiano linalokutatiza? Wasiliana nami kwa ujumbe mfupi kupitia simu ya ofisi namba 0715268581 (usipige), au barua pepe; fwingia@gmail.com au flora.wingia@guardian.co.tz

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post