SHIRIKA LA NDEGE TANZANIA KUANZISHA SAFARI ZA MOJA KWA MOJA ZAMBIA,ZIMBABWE NA CHINA Via THAILAND


Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) liko mbioni kuanzisha safari za moja kwa moja katika nchi ya Zambia, Zimbabwe pamoja na China kupitia Thailand huku ikiongeza vituo vitano vya ndani ya nchi.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk Leonard Chamuriho leo Jumapili Desemba 23,2018 katika mapokezi ya ndege mpya ya Airbus A220-300 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).

Dk Chamuriho amesema huo ni utekelezaji wa awamu ya pili ya upanuzi wa mtandao wa ATCL ikiwa ni baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza.

Amesema vituo vya ndani vitakavyoongezwa ni Mpanda, Pemba, Iringa, Kahama, Musoma na kurudisha safari za Songea na Mtwara.

“Utekelezaji wa safari hizo za ndani utatokana na kukamilika kwa utekelezaji wa ujenzi wa viwanja hivyo juu ya ujenzi wa miundombinu unaofanyika pamoja na uwepo wa abiria wa kutosha ikiwamo mbinu za kibiashara,” amesema Dk Chamuriho

Amesema utekelezaji wa awamu ya tatu ukifuatiwa na mpango mkakati wa miaka mitano utaanza 2021-2022 ambao utahusisha safari za Ghana, Nigeria, Dubai, Uingereza na Muscat.

“Wakati tunaanza tulikuwa na marubani 16 na hadi sasa tunao 50, wengi wao ni wale tuliowatayarisha wenyewe kupitia mpango mafunzo ya awali nchini na kuwapeleka nje ya nchi kupitia makubaliano tuliyoweka na Shirika la Ndege la Ethiopia na Kampuni ya Bombadier,” amesema Dk Chamuriho

Kwa upande wa mafundi na wahandisi wa ndege wameongezeka kutoka 31 waliokuwepo Oktoba 2016 hadi 87 ambapo wahandisi wazawa ni 36, wageni sita na mafundi 45 huku nafasi zikiendelea kutolewa kupitia mpango maalumu kwa vijana wa Kitanzania.

Dk Chamuriho amesema uwezo wa ndege za ATCL katika kubeba abiria umeongezeka hadi kufikia 34,000 kwa mwezi kutoka abiria 5,600 huku umiliki wa soko la ndani ukiongezeka kutoka asilimia 2 Desemba 2016 hadi asilimia 31, Oktoba mwaka huu.

Amesema shirika limepiga hatua kwa kuruka kwa ndege na kutua kwa wakati kutoka asilimia 22, Oktoba 2016 hadi asilimia 80 mwaka huu.

“Tunalipa kodi serikalini, tunawekeza katika ukodishaji pesa, hizi zote ni faida ambazo zinapatikana katika uendeshaji wa shirika hili. Tunaendelea kutumia bidhaa zinazozalishwa na kuchakatwa ndani ya nchi,” amesema Dk Chamuriho.

Amesema ndege mbili za aina hii inayopokelewa leo zilitakiwa kupokelewa Mei na Juni mwaka huu lakini kutokana na changamoto za mafundi ndiyo maana moja inapokelewa leo na nyingine Januari mwakani.

"Mpaka hivi sasa tumekuwa na vituo 11 vya huduma ambapo kimoja kipo nje ya nchi na tumeboresha mifumo ya ukataji tiketi, huduma kwa wateja na kuimarisha mifumo ya uondokaji wa ndege," amesema Dk Chamuriho.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527