DIAMOND AONESHA JEURI..AIMBA WIMBO WA NYEGEZI ULIOKATAZWA...BASATA KUKOMAA NAE

Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) limesema kitendo cha mwanamuziki Diamond Platnumz kuimba wimbo wa Mwanza uliofungiwa na baraza hilo ni dharau na kubainisha kuwa litatoa tamko kuhusu kitendo hicho.

Diamond aliimba wimbo huo alioshirikishwa na Rayvanny jana Desemba 15, 2018 katika tamasha la Wasafi lililofanyika jijini Mwanza, huku maelfu ya mashabiki wakimshangilia na kumfuatisha alivyokuwa akiimba.

Mkali huyo wa Bongo Fleva aliimba wimbo huo jukwaani akiwa pamoja na Rayvanny.

Akizungumzia na Mwananchi kuhusu kitendo hicho leo Jumapili Desemba 16, 2018 katibu mtendaji wa Basata Godfrey Mngereza amesema, “Nimepigiwa simu kuhusu hii kitu. Niko Arusha kikazi nimeshawasiliana na mwenyekiti wa bodi (ya Basata).”

“Basata itakuja na majibu muafaka kwani hapa (Diamond) kaonyesha kiwango cha juu cha dharau kwa baraza, bodi, wizara (Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo) na Serikali kwa ujumla.”

Wimbo huo ulifungiwa Novemba 12, 2018 na baraza hilo kwa maelezo kuwa unahamasisha masuala yasiyokubalika katika jamii.

Akizungumza wakati akitoa tamko la kufungiwa kwa wimbo huo Mngereza alisema hautakiwi kuchezwa mahali popote.


Alipoulizwa kama ni ruksa wimbo huo kupigwa katika tamasha la Wasafi lililoanza Novemba 24, 2018 likifanyika mikoa mbalimbali nchini Tanzania, alisema nalo watalifungia iwapo watautumia wimbo huo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527