WAZIRI MKUU APOKEA RIPOTI YA UCHUNGUZI AJALI YA MV NYERERE

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea ripoti ya uchunguzi wa ajali ya kivuko cha MV Nyerere kutoka kwa kamati iliyoundwa na Serikali kwa ajili ya kuchunguza ajali hiyo.

Amepokea ripoti hiyo leo (Alhamisi, Oktoba 25, 2018) kutoka kwa Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Mstafu, Jenerali George Waitara,kwenye makazi ya Waziri Mkuu, jijini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuishikuru kamati hiyo kwa niaba ya Rais Dkt. John Magufuli kwa kazi kubwa waliyoifanya ambayo imethibitisha umakini wao.

Pia ameipongeza kamati hiyo kwa namna walivyotumia muda wao vizuri kwa kufanya kazi hiyo na kutoa mapendekezo kwa Serikali juu ya mambo waliyoyabaini.

“Nimepokea taarifa kwa niaba ya Serikali, Serikali itafanya mapitio ya taarifa yote na viambatisho vyake na itapitia kwa kina mapendekezo mliyoyatoa ambayo yote yatafanyiwa kazi.”

Waziri Mkuu ameongeza kuwa Serikali inaamini mambo yote yaliyosheheni katika taarifa hiyo ni yale ambayo Watanzania wanasubiri kuona yakifanyiwa kazi.

MV Nyerere ilipindika na kuzama Septemba 20, mwaka huu katika ziwa Victoria ambapo Watanzania zaidi 200 walipoteza maisha na wengine Zaidi ya 40 waliokolewa.

Septemba 24 mwaka huu Waziri Mkuu alitangaza kamati ya kuchunguza ajali ya kivuko cha MV Nyerere yenye wajumbe saba ambayo iliyoongozwa na Jenerali mstaafu, Waitara.

Akitangaza majina hayo kwenye kijiji cha Bwisya katika kisiwa cha Ukara, wilayani Ukerewe, mkoani Mwanza, Waziri Mkuu alisema wajumbe hao wanapaswa kuikamilisha kazi hiyo ndani ya mwezi mmoja.

Aliwataja wajumbe wengine ni aliyekuwa Mbunge wa Ukerewe, Bw. Joseph Mkundi, Mhandisi Marcelina Magesa, Wakili Julius Kalolo na Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Bi. Queen Mlozi.

Wengine ni SACP Camillus Wambura na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Uratibu Maafa katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Bw. Bashiru Taratibu Hussein.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
ALHAMISI, OKTOBA 25, 2018.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527