MCT YAIKABIDHI MANISPAA YA SONGEA MRADI WA BILIONI 1.2

Shirika la Miracle Corner Tanzania (MCT) limeikabidhi Manispaa ya Songea eneo la ardhi yenye ukubwa wa hekari 50, lenye mradi wenye thamani ya shilingi Bilioni 1.2 unaojihusisha na utoaji wa huduma ya afya ya kinywa na meno na huduma za kijamii katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.

Akizungumza katika makabidhiano hayo yaliyofanyika siku ya Jumatano Oktoba 24,2018 katika ofisi ya Mstahiki Meya Manispaa ya Songea, Mwenyekiti wa bodi ya MCT Bi. Halima Mamuya amesema licha ya mradi huo kurudishwa serikalini, wataendelea kushirikiana na serikali ili kuhakikisha jamii inapata huduma bora.

“Tunarudisha eneo hili ili serikali iweze kufanya vitu vikubwa zaidi, na tupo tayari kushirikiana nanyi, na programu hii ya vinywa na meno hatutaiacha, tutaendelea nayo, na eneo hili litakapokuwa hospitali tutashirikiana na ninyi katika kuliendeleza hasa katika kitengo cha kinywa na meno”, alisema Bi. Mamuya

Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea Abdull Chaweji, alisema mkakati wa serikali ni kuboresha afya kwa wananchi na kuongeza kuwa eneo hilo lipo kwenye mkakati ya kujengwa hospitali ya wilaya.

“Natambua kuwa mlifanya hivi kwa ajili ya kupambana na maradhi, halmashauri yetu na baraza la madiwani wamelipokea kwa furaha na eneo lile sasa tunaliweka maalumu kwa kuanzisha hospitali ya wilaya yetu”, alisema Chaweji.

Aidha meneja wa shirika hilo Jane Shuma alibainisha kuwa ardhi hiyo yenye ukubwa wa hekari 50 iliyopo katika eneo la Kipera walipewa na Manispaa ya Songea mwaka 2004 kwa lengo la kuanzisha huduma za kijamii, ambapo walianza kwa kujenga kliniki ya meno, ukumbi wa mikutano (community hall), maktaba na nyumba 12 za watumishi mbalimbali wanaofanya kazi katika mradi huo.

ANGALIA VIDEO HAPA CHINI


ANGALIA PICHA ZA MATUKIO HAPA CHINI
Mwenyekiti wa bodi ya MCT Bi. Halima Mamuya akisaini hati ya makabidhiano, kulia ni Mstahiki Meya wa Manispaa Ya Songea Abdull Chaweji.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea, Abdull Chaweji akishuhudia zoezi la utiaji saini hati ya makabidhiano.
Meneja Wa Shirika la MCT, Bi Jane Shuma akisaini hati ya makabidhiano.
Kulia ni Meneja wa Shirika la MCT Bi. Jane Shuma, katikati ni Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea Abdull Chaweji na kushoto ni Mwenyekiti wa bodi ya MCT Bi. Halima Mamuya wakiwa katika ofisi ya Mstahiki Meya Manispaa ya Songea wakati wa kusaini hati ya makabidhiano.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea (kulia) akipeana mkono wa heri na Mkurugenzi wa programu Afrika (MCW) Bi.Regina Leichner
Moja kati ya vifaa vinavyopatikana katika kliniki ya kinywa na meno,
Moja ya jengo lililopo katika mradi uliokabidhiwa na MCT kwa serikali.
Picha ya pamoja baada ya kusaini hati za makabidhiano

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527