KIVULINI YAENDESHA KIKAO KUJADILI UTEKELEZAJI WA MPANGO MKAKATI WA TAIFA WA KUTOKOMEZA UKATILI DHIDI YA WANAWAKE NA WATOTO (MTAKUWWA)

Shirika La Kivulini la Jijini Mwanza limeendesha Kikao cha kujadili utekelezaji wa Mpango Mkakati Wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA).

Kikao hicho kilichowashirikisha watendaji mbalimbali wa ngazi ya Tarafa, kata, walimu wakuu wa shule za msingi na wawakilishi kutoka dawati la Jinsia wilayani Shinyanga kimefanyika leo Jumanne Oktoba 23, 2018 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.

Akifungua kikao hicho,mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Hoja Mahiba alisema suala la ukatili wa kijinsia, mimba na ndoa za utotoni bado ni changamoto katika halmashauri hiyo ya wilaya na kwamba kila mdau anapaswa kusimama kidete kupiga vita vitendo hivyo.

“Kuwepo kwetu hapa leo hii tutambue kuwa tunaguswa moja kwa moja katika suala zima la kupambana na ukatili wa kijinsia, iwe ni wakuu wa idara, walimu wakuu, watendaji wote, lazima tujipime tuone iwapo tunatosha kwenye nafasi zetu tulizonazo.

"Ukiona mambo hayaendi vizuri ni wazi hautoshi kwenye nafasi uliyonayo, tuwe makini kuzingatia mafunzo tunayopatiwa na baada ya hapa tukayatekeleze huko kwenye maeneo yetu",alisema.

"Tufike sehemu halmashauri yetu isiwe na kesi za mauaji ya kikatili ya wanawake vikongwe, tukae tujiulize, kwa nini Shinyanga, tukilielewa tatizo lazima tutafanikiwa,” alieleza Mahiba. 

Kwa upande mwingine Mahiba alikemea tabia ya baadhi ya maofisa watendaji wa kata kuwaficha watuhumiwa wanaobainika kuwapa mimba watoto wa shule ama kuoa wanafunzi na badala yake wahakikishe wanafikishwa mikononi mwa vyombo vya dola.

“Ni muhimu hivi sasa tukaanza upya, tusahau yale yaliyopita, tuanze ukurasa mpya kwa kuongeza bidii kwenye kupiga vita vitendo vyote vya ukatili na tuhakikishe leo hii tunatoka na mikakati ya kupambana na vitendo hivi,” alieleza Mahiba.

Ofisa maendeleo ya jamii mkoani Shinyanga, Glory Mbia, alisema mkoa wa Shinyanga ni miongoni mwa mikoa sita nchini ambayo bado ina kiwango cha juu cha vitendo vya ukatili ikiwemo mimba na ndoa za utotoni.

Alisema kutokana na hali hiyo kuna kila sababu ya kuhakikisha kila mmoja anasimama imara katika kupiga vita vitendo vya mimba na ndoa za utotoni ikiwemo suala la utoro kwa wanafunzi mashuleni.

"Niwaombe kuhusu uwekaji vizuri wa takwimu zetu, hasa taarifa za mimba kwa wanafunzi mashuleni, maana katika halmashauri yetu takwimu hizi haziko vizuri",alisema.

"Lazima tuhakikishe takwimu zetu za masuala ya ukatili zinakaa sawa tofauti na hali ilivyo hivi sasa, maana kila sehemu ukienda unakutana na takwimu tofauti iwe polisi ama kwenye ofisi za watendaji wa kata",aliongeza

Kiwango cha ukatili kwa wanawake kwa mkoa wa Shinyanga kinatajwa kuwa asilimia 75 hivyo juhudi zinahitajika kushusha kiwango hicho ili kufikia angalau asilimia 70.

Naye mratibu wa Shirika la Kivulini, Eunice Mayengela alisema jukumu la kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia ni la watu wote hasa watendaji wa serikali ambao ndiyo kimbilio la wanyonge.

“Ni muhimu sisi sote tukachukia vitendo hivi vya ukatili vinavyofanyika kwenye maeneo yetu, na tukubali kubadilika hasa kwa maofisa watendaji wa kata waache tabia ya kuwaficha watuhumiwa wanaokamatwa na badala yake wafikisheni kwenye vyombo vya dola,” alieleza.

Wakichangia mada washiriki wa mafunzo hayo wamesema ni vizuri kesi zinazohusiana na masuala ya ukatili wa kijinsia, mimba na ndoa za utotoni ziwe zinasikilizwa kwa wakati na zifikishwe mahakamani badala ya kuishia polisi.

Pia wameshauri Jeshi la Polisi kuharakisha kuwakamata watuhumiwa wanaodaiwa kuwapa mimba wanafunzi, badala ya kusubiri taratibu za vikao hali inayotoa fursa kwa watuhumiwa kutoroka. Hali hii imeelezwa kuwa kikwazo katika kuwakamata wahalifu.

Kwa upande mwingine washiriki hao walisema ni vizuri pakawepo na mshikamano wa karibu miongoni mwa watumishi wa serikali, maofisa watendaji vijiji, kata na walimu na Jeshi la Polisi katika kuwashughulikia watu wanaofanya vitendo vya ukatili ikiwemo kuwapa mimba wanafunzi.

Mwakilishi wa Dawati la Jinsia, Rahma Swalehe alisema hakuna kesi inayocheleweshwa na polisi bali hali hiyo huchangiwa na jalada kuchelewa kurejeshwa kutoka kwa mwanasheria wa serikali na mara nyingi jamii husika haipendi kutoa ushirikiano kutokana na kukataa kutoa ushahidi.

Wakihitimisha kikao hicho washiriki walipitisha maazimio kadhaa ikiwemo suala la kuandaa mpango kazi wa jinsi ya kushughulikia masuala ya kupiga vita vitendo vya ukatili na uundaji wa kamati za MTAKUWWA kwa kila ngazi husika.

Moja ya majukumu ya kamati ngazi ya Halmashauri yaliyojadiliwa katika kikao hicho ni pamoja kuhakikisha utekelezaji wa mpango kazi ngazi ya Taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto na shughuli za utoaji huduma kwa makundi yaliyo katika mazingira hatarishi ili uendane na mikataba ya kikanda na kimataifa ya Haki na Ustawi wa wanawake na watoto pamoja na sera, sheria na miongozo ya serikali.

Na Suleiman Abeid - Malunde1 blog
Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Hoja Mahiba akifungua kikao cha kujadili utekelezaji wa Mpango Mkakati Wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA).
Washiriki wa kikao wakiwa ukumbini
Ofisa maendeleo ya jamii mkoani Shinyanga, Glory Mbia akizungumza wakati wa kikao hicho
Mratibu wa Shirika la Kivulini, Eunice Mayengela akiwa ukumbini.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post