WAKULIMA KOROGWE WAELEZA WALIVYONUFAIKA NA MKONGE NA MAZAO MENGINE


Baadhi ya mashine za kulainishia singa (brashi) maarufu kama Kayamba kwenye Shamba la Mkonge Magoma (Kulasi). (Picha na Yusuph Mussa).

BAADHI ya wakulima wa mkonge Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga wamesema tangu wamegawiwa mashamba kwa ajili ya kilimo hicho kupitia mfumo wa Wakulima wa Mkonge (SISO), wamepata faida nyingi ikiwemo kulima mkonge na mazao mengine kwa wakati mmoja.

Kupitia mfumo wa SISO ambao uliasisiwa na Kampuni ya Katani Ltd mwaka 1998, umewapa faida, kwani kampuni hiyo iliwapa elimu kuwa wakitaka kufanikiwa, basi walime mkonge huku wakichanganya na mazao mengine kwa miaka mitatu ya kwanza.

Waliyasema hayo Oktoba 21 kwa nyakati tofauti, kwenye mahojiano na mwandishi wa habari hizi katika Shamba la Mkonge Magunga, ambapo walikuwa wanaelezea mafanikio waliyopata kwa miaka 20 ya Mfumo wa SISO, ambao kwa kiasi kikubwa umeleta mafanikio kwenye mashamba ya mfumo huo ambayo ni Mwelya, Magoma, Magunga, Hale na Ngombezi.

"Moja ya mafanikio tuliyopata katika mfumo wa SISO ni elimu tuliyokuwa tunapewa mara kwa mara ili tuweze kulima kwa ufanisi. Na elimu hiyo ilipita kwa kila mkulima kuwa pamoja na kupanda mkonge, lakini hakikisheni mnalima mazao mengine ndani ya mkonge, hiyo imetusaidia sana kujitosheleza kwa chakula na mahitaji mengine.

"Kutokana na hilo, wakulima wengi walihamasika kulima mkonge na mazao mengine na wakaiona faida yake. Lakini ili kuwa na uhakika na mashamba ambayo kila mmoja alishamegewa kipande chake, basi Serikali utugawie Hati Miliki ya mashamba hayo, kwani itatusaidia kupata mikopo ya muda mrefu na mfupi, kwani zao la mkonge mpaka kuja kuvuna inakuchukua kati ya miaka mitatu hadi mitano, hivyo ni uwekezaji wa muda mrefu", alisema Willy Homange.

Nae mkulima Michael Mweta wa Magoma, tangu mwaka 2002 amekuwa analima mkonge, na moja ya faida alizopata kwa kujitosa kwenye kilimo hicho ni kusomesha watoto na kujenga nyumba, lakini pia ameweza kuwasaidia wananchi wanaozunguka kwenye maeneo hayo ya mashamba kwa kuwapa ajira.

"Mkulima wa mkonge anatoa ajira kwa watu wengi kuanzia kulima, kupanda, kukata mkonge, kubeba na kupeleka kwenye korona. Bado kuna wanaolisha mkonge kuanika, kuanua, kulainisha singa (brashi) kwenye kayamba, kufunga robota (Press) hadi kusafirisha sokoni", alisema Mweta.

Mkulima mwingine wa Magunga, Theodora Mtejeta alisema kilimo cha mkonge kimempa faida nyingi ikiwemo kuendesha maisha yake yeye, watoto wake na wajukuu, kwani wote wamepata elimu kwa ajili ya mkonge, hivyo unapozungumzia mkonge, unazungumzia maisha ya wananchi wa Tanga.

"Watu hawajui kuwa mkonge ulikuwa ni zao la kwanza kuingiza fedha nyingi kwenye Pato la Taifa (GDP) mwaka 1970. Mkonge uliingiza Pato la Taifa kwa zaidi ya asilimia 60, hivyo mkonge ulilisha nchi kwa miaka 10. Na kwa heshima hiyo Nembo ya Benki Kuu (BoT) ina alama ya mkonge. Hivyo mkonge ni zao la kuenziwa na kuendelea kulijengea uwezo liendelee kuwasaidia wananchi wa Tanga na Taifa kwa ujumla", alisema Mtejeta.

Mkulima, mfanyabiashara na mfanyakazi wa Katani Ltd Shamba la Mkonge Magunga, Margareth Gosi alisema, tangu kufungwa kwa Kiwanda cha Mkonge Magunga zaidi ya miezi miwili sasa ili kupata muafaka wa maslahi kati ya wakulima na Katani Ltd, wakulima wa mfumo wa SISO na wafanyakazi wa Katani Ltd wameathirika kwa kiasi kikubwa.

"Mimi hapa ni mfanyakazi, lakini pia nalima mkonge, na vile vile ni mfanyabiashara. Nimeathirika sana. Kwanza hakuna mshahara, na biashara yangu inaendeshwa na mshahara. Nimeshindwa kutuma pesa za VICOBA wala za NSSF, hivyo kuifanya Bima ya Afya kupitia NSSF isifanye kazi, kwani usipolipia miezi mitatu mfululizo, huduma ya bima kupitia NSSF inasitishwa kwa muda.

"Bado tuna imani na Serikali pamoja na Waziri wa Kilimo (Dkt. Charles Tizeba), ambaye alisema ndani ya siku 14 kuanzia Septemba 25 hadi Oktoba 9, mwaka huu, atakuwa ameshapata muafaka wa wakulima wa mkonge na Katani Ltd na uzalishaji uweze kuanza" alisema Gosi.

Na Yusuph Mussa-  Korogwe

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post