WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA AMPONGEZA MWAKINYO KUMCHAPA MWINGEREZA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amempongeza mwanamasumbwi wa Kitanzania Bw. Hassan Mwakinyo (23) kwa kumchapa bondia Mwingereza Bw. Sam Egginton.


Bw. Mwakinyo alimchapa Bw Egginton kwenye raundi ya pili ya pambano lao la masumbwi lililofanyika Jumapili, Septemba 9, 2018, huko Birmingham nchini Uingereza.


Waziri Mkuu ametoa pongezi hizo leo (Ijumaa, Septemba 14, 2018) wakati akiahirisha mkutano wa 12 wa Bunge, Bungeni jijini Dodoma. Bunge limeahirishwa hadi Novemba 6, 2018.


Amesema bondia huyo amelipa Taifa heshima kubwa kwa kulitangaza kimataifa katika Nyanja ya michezo, hivyo amewataka wanamichezo wengine nchini waige mfano wake.


Wakati huo huo, Waziri Mkuu ameipongeza timu ya Taifa ya Wanawake (Kilimanjaro Queens) kwa kutwaa kombe la Afrika Mashariki.


Pia ameipongeza timu ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) kwa kuwa washindi wa tatu kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kwenye mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF). 


“Hongereni sana wanamichezo wetu na endelezeni moyo huo wa kizalendo mliouonesha katika kulitangaza Taifa letu.


Pia Waziri Mkuu amesema mwaka 2019 Tanzania itakuwa mwenyeji wa mashindano ya mpira wa miguu kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 (AFCON-U17) yanayoandaliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika.


Amesema hiyo ni fursa nyingine ya kipekee ya kulitangaza Taifa letu katika nyanja za Kimataifa, hivyo Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inaendelea na maandalizi, ambayo yatahusisha ukarabati wa viwanja vitakavyotumika katika mashindano hayo.


Waziri Mkuu ametoa wito kwa wananchi watumie vizuri uwepo wa mashindano hayo kujiongezea kipato hususan kupitia biashara ya bidhaa na huduma kwa wageni, pia amewataka wawe wazalendo kwa kuunga mkono timu zinazoshiriki mashindano ya Kimataifa ili zipate mafanikio.


IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527